1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya Kimataifa yataka mapigano Gaza yasitishwe.

Sekione Kitojo30 Desemba 2008

Jumuiya ya kimataifa imetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano katika ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo .

https://p.dw.com/p/GPBY
Wazima moto wa Palestina wakijaribu kuzima moto katika jengo moja lililokuwa likitumika na jeshi la usalama la Hamas baada ya kushambuliwa na jeshi la Israel.Picha: AP

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon ametaka mapigano yasitishwe haraka iwezekanavyo katika ukanda wa Gaza na kuwataka viongozi wa mashariki ya kati na dunia kwa jumla kuchukua hatua zaidi kusaidia kumaliza mzozo kati ya Hamas na Israel na kuhimiza majadiliano ya kisiasa.




Baada ya kikao cha faragha siku ya Jumapili usiku, baraza la usalama la umoja wa mataifa lenye wajumbe 15 lilitoa taarifa ya kisiasa isiyokuwa na ukali , ikieleza tu wasi wasi mkubwa kuhusiana na mashambulio yenye athari kubwa ya Israel dhidi ya Gaza na kutoa wito wa kusitisha mara moja kwa ghasia hizo.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon alizungumza jana , ikiwa ni siku ya tatu ya mashambulio ya ndege ya jeshi la Israel dhidi ya Gaza ambayo yamesababisha vifo vya watu karibu 360 ikiwa ni pamoja na wanawake 62 na watoto kwa mujibu wa umoja wa mataifa na kujeruhi kiasi cha watu 1,400.

Ban ametaka kusitishwa mara moja kwa mapigano hayo.Ameongeza Ban kuwa washirika wa kimkoa na kimataifa hawajafanya vya kutosha. Katibu mkuu pia amezitaka nchi za Kiarabu , ambazo zinakutana kwa kikao cha dharura kesho Jumatano , kuchukua hatua za haraka ili kumaliza hali hii ya mkwamo.

Pia amewataka viongozi wengine duniani kuongeza juhudi za kuunga mkono suluhisho la muda mrefu la suala hilo.

Kansela wa Ujerumani ameonya kuwa mzozo huo utaongezeka zaidi katika mashariki ya kati. Akizungumza kwa simu na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert kansela Angela Merkel ameungana na waziri mkuu huyo kuwa Hamas inabeba lawama zote za mzozo huu, kwa mujibu wa maelezo ya msemaji wa serikali Thomas Steg.

Serikali ya Ufaransa jana imetoa wito wa mkutano wa dharura wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya ili kujadili mzozo huo katika mashariki ya kati wamethibitisha maafisa wa Ufaransa. Ufaransa ambayo inashikilia urais wa umoja huo kwa sasa imeitisha mkutano huo wa mjini Paris leo Jumanne ili kujadili mchango wa umoja wa Ulaya katika kutatua mzozo uliopo hivi sasa.Suluhisho litakuwa kwa ushirikiano na juhudi za kimataifa , hususan zile zinazochukuliwa na katibu mkuu wa umoja wa mataifa.

Wakati huo huo mataifa ya Kiislamu jana yameishutumu Israel kutokana na mashambulio yaliyosababisha vifo vingi katika ukanda wa Gaza. Ikipuuzia miito ya mataifa ya Kiarabu, Marekani imedai kuwa Hamas wakubali kusitisha mapigano , makubaliano ambayo yatakuwa ya kudumu na endelevu, na kueleza uungaji wake mkono kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya eneo la Gaza.