1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa yawashinikiza viongozi wa Kenya wagawane madaraka

30 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CzXd

Jumuiya ya kimataifa inamshinikiza rais Mwai Kibaki wa Kenya na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wagawane madaraka ili kuumaliza mzozo wa kisiasa uliosababishwa na matokeo ya uchaguzi.

Jana Kofi Annan alianzisha rasmi mazungumzo ya kuutanzua mzozo wa kisiasa kati ya rais Mwai Kibaki na Raila Odinga mjini Nairobi. Rais Kibaki amesema mchakato wa mdahalo wa kitaifa umeanza ili kuishughulikia hali ya kisiasa nchini Kenya.

Akizungumza mjini Nairobi Kofi Annan amesema ana matumaini maswala ya kisiasa yanayohitaji kutatuliwa yatapatiwa ufumbuzi katika majuma manne yajayo na kuipa Kenya mwaka mmoja kukabiliana na uharibifu uliosababishwa na machafuko ambapo watu takriban 1,000 wameuwawa.

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umelaani vikali mauaji ya mbunge wa upinzani, Mugabe Were, aliyeuwawa mapema jana wakati alipokuwa akirejea nyumbani kwake mjini Nairobi. Umoja huo pia umeitaka serikali na upinzani ushirikiane na Kofi Annan kuumaliza mgogoro wa kisiasa uliopo.