1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juncker aeleza matumaini baada ya Brexit

Sekione Kitojo
13 Septemba 2017

Rais wa halmashauri ya Umoja  wa Ulaya Jean-Claude Juncker amesema upepo umerejea katika "matanga ya chombo cha Ulaya" wakati akitoa wito wa kuwa pamoja mwaka mmoja baada ya kura iliyotikisa umoja huo nchini Uingereza.

https://p.dw.com/p/2jraa
Straßburg Rede von Jean-Claude Juncker
Picha: Reuters/C. Hartmann

Katika hotuba yake  ya  hali  ya  Umoja  wa  Ulaya, Juncker  amesema kundi  hilo  la  mataifa  limekuwa  na  umoja  zaidi  kufuatia  mlolongo wa  mizozo, na  kusisitiza kasi ya  kiuchumi inaanza  kuonekana. 

Waziri  mkuu huyo wa  zamani  wa  Luxembourg ameuhimiza  Umoja wa  Ulaya  kuimarisha hatua ya  mataifa  hayo  kuwa pamoja zaidi, na  pia  alisema  Umoja  huo  unapaswa  kujaribu  kufikia makubaliano  ya  kibiashara  na  Australia  na  New Zealand  ifikapo mwishoni mwa muhula  wake madarakani.

Deutschland G20 Gipfel Jean-Claude Juncker und Donald Trump
Jean-Claude Juncker akizungumza na rais wa Marekani Donald Trump (kulia)Picha: Getty Images/AFP/M. Schreiber

Juncker  alionesha  matumaini  zaidi  katika  hali  bora  ya  kiuchumi katika  mataifa  hayo  kuliko ilivyokuwa  wakati  alipohutubia  bunge hilo  la  Ulaya  mjini  Strassbourg  Septemba  2016 , akikiri  wakati huo  kwamba , "ni wazi  kwa  kila  mtu  kuona  kwamba  Umoja  wetu hauko  katika  hali  nzuri, ukivurugwa  na mwaka  ambao ulitikisa msingi wa  Umoja  huo.

Lakini wakati kuibuka  kwa  siasa kali  za  mrengo wa  kulia , baada ya  Brexit  na kuchaguliwa  kwa  rais Donald Trump nchini  Marekani , kukionekana kudhibitiwa hivi  sasa, Juncker amesema  viongozi wa mataifa  27  yaliyobakia  katika  Umoja  wa  Ulaya wamejiunga pamoja  nyuma  ya  miito  yake  ya  Umoja.

Wito wake wa  kuongeza  ushirikiano hata  hivyo  ulienda sambamba  na  haja  ya  kuponesha  mgawanyiko  mkubwa  na mataifa  ya  ulaya  mashariki  ambayo yanazuwia  hatua  yoyote zaidi  ya  ujumuisho  katika  Umoja  huo.  Juncker  alisema:

"Sasa  ni  wakati wa  kujenga Ulaya  iliyo na  Umoja  zaidi, imara na yenye  demokrasia  zaidi  kwa  ajili  ya  mwaka  2025."

Deutschland G20 Begrüßung der Teilnehmer durch Merkel
Jean-Claude Juncker akisalimiana na kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kulia)Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Waziri wa fedha wa EU

Juncker  mwenye umri wa  miaka 62 , ana chini  ya  miaka  miwili kubaki  madarakani  akiwa  mkuu  wa  chombo  hicho chenye  nguvu cha  utendaji cha  Umoja  wa  Ulaya  kuhakikisha  kwamba atakayoyaacha  sio tu  kujitoa  kwa  mwanachama  mkubwa  katika Umoja  huo.

Juncker  amesema  kuna  haja  kwa  Ulaya  kuwa  na  waziri  maalum wa  fedha, ikiwa hatua  kubwa  kuelekea kanda  ya  euro  kujumuika zaidi.

Juncker  pia  amezungumzia  kuhusu  Uturuki akisema nchi  hiyo inajitenga kutoka  Ulaya  na  haitakuwa  mwanachama  wa  kundi hilo  la  mataifa  katika  kipindi cha  karibuni.

Türkei Präsident Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan Picha: Reuters/O. Orsal

Kuhusu  wakimbizi  na  wahamiaji, rais  huyo  wa  halmashauri ya Umoja  wa  Ulaya  amesema , Ulaya  inapaswa  kuchukua  jukumu  la pamoja  kusaidia kuweka  mazingira  kuwa  bora  zaidi  katika  vituo vya  kuwahifadhi  wahamiaji  nchini  Libya. Juncker  amewaambia wabunge  wa  Ulaya  kwamba  Umoja  huo  unapaswa  kufanyakazi kwa  pamoja  na  shirika  la Umoja  wa  Mataifa  la  kuwajhudumia wakimbizi  kuhakikisha  kwamba  hali  hiyo  ya kudhalilisha haiendelei.

Pia  amesema ataomba  kupewa madaraka  kuchunguza wawekezaji wa  nje wanaotaka  kununua sekta muhimu za  kimkakati barani Ulaya, huku  kukiwa  na  wasi swasi  juu  ya  uwekezaji  wa  China barani  humo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae /

Mhariri: Iddi Ssessanga