1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juncker ataka Euro iokolewe haraka

30 Julai 2012

Mkuu wa nchi zinazounda kanda ya sarafu ya Euro, Jean-Claude Juncker, ameonya juu ya uwezekano wa kuvunjika kwa kanda ya sarafu ya Euro, na amesama kwamba ni lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kuiokoa sarafu hiyo.

https://p.dw.com/p/15gSL
Jean-Claude Juncker, mkuu wa kundi la Euro
Jean-Claude Juncker, mkuu wa kundi la EuroPicha: Reuters

Jean-Claude Juncker, ambaye pia ni waziri wa fedha wa Luxemburg, ameliambia gazeti la Süddeutsche Zeitung la hapa Ujerumani kwamba sasa umefika wakati muafaka kuthibitisha kwamba nchi zinazotumia sarafu ya Euro ziko tayari kuhakikisha uimara wa jumuiya hiyo ya kiuchumi. Juncker alisema pia kwamba ikihitajika, nchi za kanda ya Euro, mfuko wa uokozi wa Euro na benki kuu ya Ulaya zinajiandaa kununua dhamana za serikali za nchi zilizokumbwa na mgogoro wa kiuchumi.

Mwenyekiti wa chama cha Christian Social Union CSU, Horst Seehofer, ameikosoa hatua hiyo na kusema kwamba si sawa kwa benki kuu ya Ulaya kuzungumzia uwezekano wa kununua dhamana za serikali. "Haiwezekani Benki Kuu ya Ulaya iamue kuchukua hatua za uokozi katika kanda nzima ya Euro, kwa mfano katika nchi ya Uhispania," alisema Seehofer. "Ni kama vile maamuzi ya bunge la Ujerumani hayana umuhimu wowote ule." Juncker ameilaumu pia Ujerumani kwa kuingiza siasa za ndani katika maamuzi yote yanayohusu sarafu ya Euro.

Mwenyekiti wa chama cha CSU, Horst Seehofer
Mwenyekiti wa chama cha CSU, Horst SeehoferPicha: dapd

Ugiriki kupunguza bajeti

Waziri wa fedha wa Marekani, Timothy Geithner, leo anakutana na mwenzake wa Ujerumani Wolfgang Schäuble katika kisiwa cha Sylt kilichopo kaskazini mwa Ujerumani, ambapo Schäuble alikuwa akifanya likizo. Taarifa za undani kuhusu yale yatakayozungumziwa katika mkutano wa viongozi hao hazikutolewa na wizara ya fedha ya Ujerumani. Hata hivyo, inafahamika kwamba mada kuu itakuwa hali ya kiuchumi ya Ulaya na dunia kwa ujumla. Geithner Jumatatu jioni atakutana pia na rais wa benki kuu ya Ulaya, Mario Draghi.

Wakati huo huo, uchumi wa Uhispania unazidi kushuka, licha ya hatua za kubana matumizi kuchukuliwa. Bei za vyakula nazo zimepanda kwa asilimia 2.2 ikilinganishwa na bei za mwaka uliopita.

Raia wa Uhispania wakiandamana kupinga hatua za kubana matumizi
Raia wa Uhispania wakiandamana kupinga hatua za kubana matumiziPicha: Getty Images

Na huko Ugiriki, wakaguzi wa mahesabu wa Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF, wanaendelea na ukaguzi wao nchini Ugiriki na wameeleza kwamba wataendelea kubakia nchini humo hadi itakapoundwa programu ya sera za mabadiliko ya kiuchumi. Baada ya mkutano wao wa kwanza wiki iliyopita, viongozi wa kisiasa wa Ugiriki watakutana tena leo kupitisha uamuzi wa kupunguza bajeti kwa kiasi cha Euro billioni 11.6. Makato katika bajeti yataziathiri zaidi pensheni za wastaafu, sekta ya afya na fedha za misaada zinazotolewa kwa wenye kipato cha chini au wasio na ajira. Uamuzi huo umevikasirisha vyama vya wafanyakazi, lakini waziri wa fedha wa Ugiriki ameeleza kuwa makato ya pensheni hayatawaathiri wale wanaopokea pensheni ndogo.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/Reuters

Mhariri: Othman Miraji