1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juventus yainyamazisha Barcelona

Bruce Amani
12 Aprili 2017

Mshambuliaji wa Argentina Paulo Dybala alifunga mabao mawili na kumnyamazisha mwenzake Lionel Messi wakati Juventus ilisajili ushindi wa kushangaza wa 3-0 dhidi ya Barcelona

https://p.dw.com/p/2b5WV
UEFA Champions League Juventus v FC Barcelona Dybala Tor
Picha: Getty Images/M. Hewitt

Michuano ya jana iligubikwa na tukio la kutokea milipuko mitatu karibu na basi la timu ya Borussia Dortmund, hatua ambayo ilisabaishwa kufutwa mchuano kati ya timu hiyo ya Ujerumani na AS Monaco. Milipuko hiyo ilitokea wakati basi hilo lilikuwa njiani kuelekea uwanja wa Signal Iduna Park. Klabu hiyo ilithibitisha kuwa beki Marc Bartra alipata majeraha mkononi lakini akatibiwa hospitalini. Mchuano huo sasa utachezwa leo pamoja na mechi nyingine mbili.

Dybala alifumania nyavu mara mbili mapema katika kipindi cha kwanza na Giorgio Chiellini akaongeza la tatu mapema katika kipindi cha pili mjini Turin na kuiacha Juve katika udhibiti wa mchuano huo kabla ya mechi ya mkondo wa pili uwanjani Camp Nou Jumatano wiki ijayo.

UEFA Champions League Juventus v FC Barcelona  Jubel Dybala
Paulo Dybala alikuwa moto wa kuotea mbaliPicha: Reuters/G. Perottino

Baada ya kuandikisha historia wakati waliyageuza matokeo ya mabao manne kwa sifuri ya mkondo wa kwanza dhidi ya Paris Saint-Germain katika hatua ya 16 za mwisho kwa kushinda 6-1, Barcelona watahitaji kudhihirisha mchezo kama huo kama watataka kufuzu katika hatua ya nne za mwisho.

Kocha Luis Enrique aliyejawa na hasira alisema baada ya mechi hiyo kuwa waliwazawadia Juventus mabao amwili katika nusu ya kwanza, na kama kocha, kwake, hilo halielezeki. Juventus walikutana na miamba hao wa Uhispania wakati walipoteza 3-1 katika fainali ya 2015, lakini jana, waliudhibiti mchezo kwa kuwakimbiza na kuwazima washambuliaji wa wageni wao, Messi, Neymar na Luis Suarez. Hata hivyo muujiza walioufany Barca kwa PSG una maana kuwa kocha wa Juve Massimiliano Allegri hawezi kuwapuuza.

"Napenda kuwapongeza vijana hawa kwa sababu, kama timu, walicheza vyema”. Alisema Allegri, akiongeza kuwa sio rahisi kuizidi nguvu timu kama Barcelona, lakini wote walijituma na kuhakikisha kuwa hawafungwi bao, kitu ambacho ni muhimu sana kwao.

Katika mechi za leo, Bayern Munich itaialika Real Madrid katika mtanange wa kumezea mate. Kocha wa Bayern Carlo Ancelotti aliiongiza Real kutwaa kombe la Champions League mwaka wa 2014 na atakutana na aliyekuwa msaidizi wake wakati huo, kocha wa sasa wa Madrid Zinedine Zidane.

Borussia Dortmund Spieler nach Anschlag
Basi la Dortmund lililengwa katika milipikoPicha: picture-alliance/AA/I. Fassbender

Xabi Alonso, mshindi wa Kombe la Dunia la 2010, ambaye pua alishinda Kombe la Champions League 2014 kabla ya kujiunga na Bayern, atakutana na klabu yake ya zamani kwa mara ya mwisho kabla ya kuzitundika njumu mwezi Juni. Naye kiungo wa Real kiungo wa Ujerumani Toni Kross ni mwingine atakayekabiliana na waajiri wake wa zamani.

Hata hivyo, timu zote zinakosa huduma za mabeki muhimu. Mjerumani Mats Hummels ameachwa nje kutokana na maumivu ya mishipa ya kisigino hivyo Jerome Boateng na Javi Martinez watashirikiana katika safu ya ulinzi. Real Madrid watakuwa bila ya Pepe na Raphael Varane.

Katika mechi nyingine, Atletico Madrid watashuka dimbani na Leicester City ya England. Vijana hao wa kocha Diego Simeone, Atletico, wanacheza robo fainali yao ya nne mfululizo na walipoteza fainali mbili dhidi ya mahasimu wao wa mjini Madrid katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo, lazima wafahamu kuwa Leicester wanaweza kuwaduwaza, maana waliwabandua nje Sevilla na kufuzu robo fainali ikiwa ni mara yao ya kwanza kabisa kucheza katika dimba hili.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA