1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KABUL: Wanaume sita watiwa mbaroni kwa mauaji ya Mjerumani

9 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKp

Polisi nchini Afghanistan wamewakamata wanaume sita wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mjerumani, Dieter Ruebling, aliyekuwa akifanya kazi na shirika la kutoa misaada ya kiutu, German Agro Action, nchini Afghanistan.

Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 65, aliuwawa jana kwa kupigwa risasi katika wilaya ya Sayad katika mkoa wa Sar - e - Pul kaskazini mwa Afghanistan.

Wanaume hao wanazuiliwa katika mkoa huo ambako mjerumani huyo alikuwa akifanya kazi. Akizungumza kuhusu mauji hayo, msemaji wa Umoja wa Mataifa mjini Kabul, Adrian Edwards, amesema hujuma hiyo inahuzunisha.

´Tukio hili linahuzunisha. Kwa bahati mbaya linadhihirisha kwamba Afghanistan ni mazingira hatari kwa wafanyakazi wa mashirika ya misaada. Katika kisa hiki cha muhimu ni kuhakisha, katika nchi yenye utawala dhaifu wa sheria, waliohusika wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.´

Mtaalamu wa shirika la German Agro Action nchini Afghanistan, Renate Becker, amesema shambulio hilo dhidi ya wafanyakazi wa kutoa misaada lilifanywa aidha kwa sababu za kidini au kisiasa kwa sababu washambuliaji waliiba pesa kidogo na kuyaacha magari yote mawili.

Maafisa zaidi wa polisi wametumwa katika eneo hilo kuwasaka washukiwa.