1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kadhafi adhimisha miaka 40 madarakani Libya

30 Agosti 2009

Kiongozi wa Libya Moamer Khadhafi tarehe Mosi Septemba anadhimisha miaka 40 ya mapinduzi yaliomuweka madarakani na kuimarishwa kwa kuboreka uhusiano wake na mataifa ya magharibi na kuongezeka kwa ushawishi wake Afrika.

https://p.dw.com/p/JLhk
Kiongozi wa Libya Mouamer KadhafiPicha: AP

Ahadi zilizoshindwa kutimizwa kwa muda mrefu za kusonga mbele na mageuzi ya kisiasa na kiuchumi bado ni mambo yanayoburuza miguu licha ya kuwepo kwa mipango mikubwa inayoungwa mkono na mwanawe wa pili wa kiume anayetazamiwa kurithi uongozi wake Seif al- Islam.

Mitaa ya Tripoli imepambwa kwa maelfu ya taa za rangi na mamia kwa mamia ya picha za Kadhafi na mabango yenye kumsifu kiongozi huyo ikiwa ni pamoja na lile lenye kusema Tukuzo liwe kwako Oh Mtukuzaji.

Sherehe zilizopangwa kufanyika siku ya maadhimisho hayo zitahudhuriwa na viongozi wa nchi ikiwa ni pamoja na Rais mropokaji wa Venezuela Hugo Chavez lakini viongozi kadhaa wa Ulaya walioalikwa kuhudhuria sherehe hizo hawatohudhuria.

Shamra shamra hizo zinakuja wakati Libya ikizima hasira kutokana na kumpa makaribisho ya kishujaa Abdelbaset al Megrahi aliepatikana na hatia ya kuhusika na uripuaji wa ndege ya shirika la ndege la Marekani kwenye anga ya Lockerbie baada ya kuachiliwa huru kwa misingi ya huruma kutoka gereza la Scotland hapo tarehe 20 mwezi wa Augusti.

Libya ilipuuza onyo la Marekani kwamba mapokezi yoyote yale ya hadhara yanaweza kuharibu uhusiano ambao umekuwa ukiboreka tokea serikali ya Libya ilipoukana ugaidi na azma yake ya kutengeneza silaha za maangamizi hapo mwaka 2003.

Seif al-Islam alimsindikiza Megrahi hadi nyumbani kwake na shirika lake la hisani liligharamia utetezi wa kisheria wa Megrahi.

Seif al - Islam ameliambia gazeti la Scotland hivi karibuni kwamba Lockerbie ni historia yaani juu ya kuripuliwa hewani kwa ndege ya Pan Am juu ya anga ya Lockerbie nchini Scotland hapo mwaka 1998 ambapo watu 270 waliuwawa.

Amesema hatua inayofuata ni ya manufaa na biashara ya tija na Endibutg na London.Ametaka wazungumzie mustakbali kutokana na Libya kuwa ni soko lenye utajiri mkubwa.

Mtoto huyo wa Kadhafi mwenye umri wa miaka 37 amekuwa akishinikiza mageuzi makubwa ya kisiasa na kiuchumi nchini Libya ambapo akiba kubwa sana ya mafuta,vituo vya utalii na maendeleo ya kiuchumi bado kutumiliwa.

Mageuzi hayo yanataka kuandaliwa kwa katiba, kubinafsishwa kwa vyombo vya habari vilioko chini ya udhibiti wa serikali halikadhalika mpango wa maendeleo ya kiuchumi wa dola bilioni sabini.

Wakati vigogo nchini Libya ambavyo Kadhafi alianzisha nao Jamahiriya au taifa la umma hapo mwaka 1977 inaonekana kuwa hawana shauku na mabadiliko hayo wanamageuzi wanaonya kwamba yamechelewa mno kutekelezwa.

Imad Bannani mfanyabishara na kiongozi wa zamani wa chama cha Muslim Brotherhood anaonya kwamba Libya inahitaji mpango halisi wa mkakati kwamba mageuzi lazima yatekelezwe haraka kwani kusita kufanya hivyo kunaweza kuchochea ukosefu wa utulivu nchini humo.

Kisiasa Libya imeamarishwa hivi karibuni baada ya mjumbe wa Marekani kwa Sudan kusifu dhima yake katika kuleta amani huko Dafur na Uswisi kuomba radhi kwa kukamatwa kwa muda mfupi mwaka jana kwa mtoto mwengine wa kiume wa Kadhafi.

Scott Gration amesema amefurahishwa na juhudi za serikali ya Libya kusaidia kuleta utulivu Dafur na kwamba anaona Walibya wana dhima nzuri na wanaona fahari sana kuwa washirika na Walibya.

Dhima ya Libya barani Afrika imekuwa ikizidi kuongezeka tokea Kadhafi ambaye alitangazwa hapo mwezi wa Septemba mwaka 2008 kuwa 'mfalme wa wafalme' na viongozi wa jadi wa Kiafrika kuwa mwenyekiti wa nchi wanachama 53 wa Umoja wa Afrika hapo mwezi wa Februari mwaka huu.

Katika mkesha wa kuadhimisha kunyakuwa kwake madaraka Kadhafi ameandaa Mkutano wa Viongozi wa Umoja wa Afrika kujadili migogoro inayokwamisha maendeleo barani humo na njia za kumaliza mzozo wa Dafur na nchini Somalia.

Mwandishi: Mohamed Dahman

Mhariri : Munira Mohamed