1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kadhia ya Urusi yamchanganya Trump

Saumu Mwasimba
29 Mei 2017

Rais Donald Trump wa Marekani anafikiria kuibadilisha timu ya wafanyakazi wake wa ikulu na kuwaleta maafisa wake waandamizi waliosimamia mikakati ya kampeni yake.

https://p.dw.com/p/2dmSA
Donald Trump und Jared Kushner
Picha: Getty Images/AFP/M. Ngan

 Hayo yanatokana na kile kinachoonekana kama ni kushindwa kwa timu yake hiyo kuidhibiti hali ya kishindo cha mgogoro wa madai yanayohusiana na Urusi kuingilia kati uchaguzi wa mwaka 2016.

Kuongezwa kwa timu ya mawakili pamoja na kuajiriwa wataalamu wa uhusiano wa masuala ya umma kwa ajili ya kukabiliana na wimbi la kuongezeka kufichuka taarifa mbali mbali zinazoihusisha Urusi kuwa na mkono wake katika uchaguzi wa Marekani pamoja na  uwezekano kwamba yamekuwepo mafungamano makubwa ya kinyume na sheria kati ya washirika wa Kamepini ya Trump na Urusi.Rais Trump alifanikiwa kuepuka kishindo kilichosababishwa na ufichuzi wa taarifa mpya kwasababu alikuwa katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi yake tangu alipoingia madarakani.

Baada ya kurudi nyumbani Jumamosi usiku kutoka ziara yake hiyo ya siku tisa ameonekana kuwa katika hali ya kuchanganyikiwa kutokana na kuongezeka kwa ripoti ambazo zinnagusa karibu kabisa na ikulu ya White House zikimuhusisha Jared Kushner ambaye ni mkwe wake wa kiume na pia mshauri wake wa karibu zaidi.Katika  hali kama hiyo ni wazi kwamba wasaidizi katika ikulu ya Marekani wanajiandaa na uwezekano  wa kufanyika mabadiliko wakati ambapo rais anaonekana kuchanganyikiwa na kile anachokiona ni kufeli kwa timu yake ya habari na mawasiliano katika kupambana dhidi ya madai yanayoendelea kumiminika.

Donald Trump und Jared Kushner
Picha: picture alliance/AP/dpa/A. Harnik

Siku ya Alhamisi kuna mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika katika jimbo dogo la Iowa lakini mkutano huo umeakhirishwa kutokana na kile kinachoweza kuwa uwezekano wa mabadiliko katika ratiba za Trump.Taarifa za karibuni kabisa kuhusiana na suala la Urusi zinasema kwamba Kushner alizungumza na balozi wa Urusi nchini Marekani kuhusu kuanzisha kituo cha siri cha mawasiliano kati ya Marekani na Urusi wakati wa kipindi cha rais cha mpito.

Wakati akiwa nje ya nchi mwanasheria wa muda mrefu wa rais Trump Marc Kasowitz alijiunga na timu ya kisheria ambayo bado inaendelea kuundwa  kwa ajili ya kumsaidia rais huyo katika sekeseke hili la uchunguzi ambalo linazidi kufukuta.Wanasheria wengine zaidi wanatarajiwa kujumuishwa kwenye timu hiyo sambamba na wataalamu wanaohusika na masuala ya mawasiliano ya dharura kwa lengo la kuisaidia ikulu katika kipindi cha wiki kadhaa zijazo.

G7 Gipfeltreffen in Taormina Italien US-Präsident Donald Trump
Picha: Reuters/D. Martinez

Jack Quinn ambaye amewahi kuwa mshauri wa ikulu ya White House chini ya rais wa zamani Bill Clinton anasema kwahivi sasa utawala wa Trumop unahitaji kulizima suala hili na kuuweka uchunguzi huu unaoendelea chini ya timu nyingine ya wataalamu wa shughuli za mawasiliano.Wakati wa uchunguzi wa kadhia ya Monica Lewinsky  ikulu ya Marekani chini ya Clinton ililazimika kuwajumuisha wanasheria maalum na kuunda timu maalum inayokabiliana na vyombo vya habariu  katika kulidhibiti suala zima la uchunguzi kuhusiana na kadhia hiyo na kwahivyo hawakuzitenga  kikamilifu agenda za rais na kwa mantiki hiyo Quinn anasema hilo lilikiuwa jambo lililosaidia kwa kiasi kikubwa.

Na kwa mujibu wa mtu mmoja aliyeko karibu sana na shughuli za rais Trump anaamini kwamba anachokikabili rais huyo ni zaidi ya tatizo la mawasiliano kuliko kisheria licha ya uchunguzi kupamba moto.Mtu huyo hakutaka kutajwa jina.Kishindo kwa Trump ni kikubwa mno hali ambayo hivi sasa inamlazimu kuongeza nguvu kazi ya kisheria kutoka nje.Ameshamuingiza rasmi aliyekuwa meneja wake aliyemsaidia kwenye kampeini Corey Lewandoski pamoja na naibu Kampeini maneja wake wa zamani David Bossie. Kurudi kwa Lewandoski lakini ndo haswa kilinachoangaliwa kwa macho mawili kutokana na kwamba Trump binafsi alimtimua baada ya kukorofishana na wafanyakazi wenzake  pamoja na mtoto wake mkubwa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman