1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamati ya Bunge Brazil yaunga mkono kung'atuliwa Rousseff

12 Aprili 2016

Rais wa Brazil Dilma Rousseff anakabiliwa na hatari ya kufunguliwa mashtaka baada ya kamati ya bunge jana kupiga kura ya kuuendeleza mchakato ambao huenda ukamwondoa madarakani kiongozi huyo aliyeongoza kwa mihula miwili

https://p.dw.com/p/1ITdu
Brasilien Kongress fordert Amtsenthebungsverfahren gegen Dilma Rousseff
Picha: Getty Images/AFP/E. Sa

Kamati maalumu ya bunge la congress, imepiga kura iliyoidhinishwa na wabunge 38 kati ya 27 waliopinga mchakato wa kumshtaki rais huyo. Pande zote mbili zilibeba mabango na kupiga kelele wakati zoezi la kura likikamilika baada ya saa nyingi za mjadala wenye hisia kali ambao mara nyingine uligeuka kuwa mchuano wa kurushiana maneno, hali iliyoashiria migawanyiko mikali iliyopo nchini Brazil.

Ombi hilo sasa litajadiliwa bungeni siku ya Jumapili. Ikiwa thuluthi mbili ya wabunge katika bunge hilo lenye viti 513 wataunga mkono pendekezo hilo, Rousseff ataondolewa madarakani kwa siku 180 huku baraza la Seneti likilichunguza suala hilo. Rousseff anatuhumiwa kwa udanganyifu wa fedha za bajeti muda mfupi kabla ya uchaguzi wa mwaka wa 2014 ili kuficha kiwango halisi cha nakisi ya bajeti.

Brasilien Präsidentin Dilma Rousseff
Rousseff anakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedhaPicha: picture-alliance/dpa/F. Bizerra Jr.

Baadhi ya viongozi wa upinzani wamemtangaza Rousseff kuwa alikwisha fariki kisiasa tangu chama cha Temer cha PMDB, ambacho ni kikubwa zaidi nchini Brazil, kilipojiondoa katika serikali yake ya muungano na kujiunga na wapinzani wanaotaka rais huyo avuliwe madaraka.

Hata hivyo, Rousseff, ambaye aliteswa kizuizini wakati utawala wa kiimla wa kijeshi nchini Brazil, amepambana akisaidiwa na mshirika wake na rais wa zamani Luiz Inacio Lula da Silva, ambaye anaongoza mashauriano mapana ya kujaribu kuuvunja mchakato wa kuondolewa madarakani rais. Akiwahutubia maelfu ya wafuasi jana jioni mjini Rio, Lula da Silva alisema “viongozi wa mapinduzi” wanajaribu kumwondoa madarakani rais aliyechaguliwa kwa njia huru na wananchi.

Uchunguzi wa maoni ya karibuni wa wabunge 513 uliofanywa jana na gazeti la Estadao umeonyesha kuwa 298 kati yao wanaunga mkono pendekezo hilo – ikiwa ni chini ya wabunge 342 wanaohitajika ili kuupitisha mswada huo – huku 119 wakiupinga na 96 wakiwa bado hawajafanya uamuzi.

Kwa sasa anapigana vikali kupata kura za kutosha za kumuepusha kung'olewa ofisini au kuwashawishi wabunge kususia kikao cha kuujadili mswada huo. Ikiwa bunge litapitisha mswada huo na kuukabidhi baraza la seneti, Rousseff ataondolewa madarakani kwa siku 180 wakati kesi ikiendelea. Makamu wake wa rais, Michel Temer, ambaye amejiunga na upinzani, atachukua uongozi. Temer ataweza pia kubakia kuwa rais ikiwa thuluthi mbili ya wabunge katika baraza la Seneti watapiga kura ya kumng'atua Rousseff.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo