1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kambi ya Nahr al-Bared yakimbiwa

P.Martin23 Mei 2007

Mapambano yaliyozuka kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wenye siasa kali nchini Lebanon yameua hadi watu 80.

https://p.dw.com/p/CHDs

Lakini majeshi ya serikali siku ya Jumanne yalijitolea kusimamisha mashambulizi yake kwa sababu za kiutu.

Umoja wa Mataifa umesema,kiasi ya watu 15,000 walitumia fursa hiyo kuikimbia kambi ya wakimbizi ya Nahr al-Bared,ambako vikosi vya serikali na wanamgambo wa Fatah al-Islam walipambana kwa siku tatu kwa mfululizo.

Kwa mujibu wa Hoda Samra,alie msemaji wa tawi la UNRWA,linalohudumia wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Kati,hali ya maisha kambini ni mbaya.Aliieleza hivi:

“Kila dakika hali ya kiutu inazidi kuwa mbaya.Tangu jana usiku,kuna wakimbizi wengi mno.Inasemekana kuwa maelfu ya watu wanajaribu kuikimbia kambi ya Nahr-al Bared na kwenda kambi ya jirani ya Baddawi au shule ya UNRWA mjini Tripoli.”

Wakati huo huo mashirika ya misaada yameonya juu ya maafa ya kiutu kama uhaba wa maji na chakula.Mashirika hayo yanajitahidi kama iwezekanavyo,kuwasaidia wakimbizi wanaoendelea kumiminika katika shule na vituo vya mashirika ya misaada.

Ingawa hakuna risasi iliyofyatuliwa tangu Jumanne jioni,duru za kijeshi zinasema,tatizo bado halijatenzuliwa.Duru hizo zikaongezea,kuwa tatizo hilo litamalizika,baada ya kuwateketeza wanamgambo.Matamshi hayo yanalingana na amri iliyotolewa na serikali kwa vikosi vyake.Mbunge Ahmed Fatfat alisema:

“Uamuzi ni dhahiri.Tutapigana mpaka mwisho kumaliza tatizo hilo.Tunaungwa mkono na vyama vyote vya Kipalestina na nchi za Kiarabu”.

Wakati huo huo waziri Fatfat akaeleza kuwa kuna kama raia 25,000 wa Kipalestina katika kambi ya Nahr al-Bared,wasio husika kabisa na kundi la Fatah al-Islam.Ili kuzuia vifo na majeruhi,jeshi linakwenda hatua kwa hatua na hivyo ndio hupitisha uamuzi wake.

Kwa upande mwingine msemaji wa Fatah al-Islam hii leo alieleza kuwa wanaheshimu hatua ya kuweka chini silaha lakini hawatojisalimisha.Msemaji huyo aliongezea kuwa raia wote wana uhuru wa kuondoka kambi hiyo na hakuna atakaezuiliwa.Tangu Jumapili,kiasi ya wanamgambo 300 wa kundi hilo wamejificha katika kambi ya wakimbizi ya Nahr al-Bared.

Uhusiano kati ya serikali ya Lebanon na wakimbizi wa Kipalestina umeathirika upya,tangu kambi ya Nahr al-Bared kushambuliwa na majeshi ya serikali kwa siku tatu kwa mfululizo.Wapalestina wanazidi kuhamaki,hali ya maisha inapozidi kuwa mbaya.