1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kambi ya wakimbizi ya Calais yakongolewa

Oumilkher Hamidou22 Septemba 2009

Wakimbizi 278 wakamatwa kaskazini mwa Ufaransa

https://p.dw.com/p/JmDK
Wakimbizi watiwa mbaroni na polisiPicha: AP

Polisi ya Ufaransa imekongoa hii leo kambi kubwa ya wakimbizi,mashuhuri kwa jina la "msitu" katika mji wa mwambao wa Calais,kaskazini mwa Ufaransa.Mamia ya wakimbizi na hasa wa kutoka Afghanistan, wanaosubiri fursa ya kuingia Uengereza kinyume na sheria wamejificha katika kambi hizo zilizoenea katika eneo hilo.

Katika opereshini hiyo iliyodumu saa mbili,wakimbizi 278 wamekamatwa,132 kati yao wana umri wa chini ya miaka 18-na takriban wote ni wanaume wanaotokea Afghanistan.

Kabla ya opereshini hiyo kuanza,wakimbizi kati ya 700 hadi 800 walikua wakiishi katika kambi hiyo ya msituni.Kwa mujibu wa mashirika ya huduma za kiutu,wengi wao walitoroka wiki za nyuma ili kuepuka wasikamatwe.

Uamuzi unaotatanisha wa kukongoa kambi hizo ulipitishwa wiki iliyopita na waziri wa masuala ya uhamiaji wa Ufaransa Eric Besson.

Magari ya polisi yalianza tangu saa moja za asubuhi kuizingira kambi hiyo iliyojaa vibanda vya maturubali,mabati na mabango,iliyoko katika mji wa viwanda karibu na bandari ya Calais.

Vikosi vya usalama vilipoanza kujongelea,wanaharakati wa No Boarder- Hakuna mipaka- shirika linalopambana na mitindo ya kukaguliwa wahamiaji-waliingilia kati kuwakinga wahamiaji wasimakatwe.Polisi ilitumia nguvu kuwatimua wanaharakati hao.Kwa mujibu wa ripota wa shirika la habari la Ufaransa-AFP,watano kati ya wanaharakati hao wamekamatwa.

Kwa mujibu wa mashirika ya huduma za kiutu wakimbizi, hao wa kutoka Afghanistan wamepelekwa katika kituo maalum wanakoshikiliwa wahamiaji kinyume na sheria na vijana wadogo wakapelekwa katika vituo vya mapokezi.

"Opereshini kubwa kabisa :Hii ni kambi muhimu iliyovunjwa hii leo na nyengine pia zitakongolewa siku zijazo" amesema waziri wa masuala ya wahamiaji Eric Besson aliyeongeza tunanukuu-"Msitu huu ni kituo cha wanaosafirisha watu kinyume na sheria.Si kambi ya kiutu.Kuna wahalifu-ni mahala ambapo "kanuni za mwenye nguvu mpishe" ndizo zinazotawala."Mwisho wa kumnukuu waziri wa masuala ya wahamiaji Eric Besson.

Frankreich EU Straßburg Finanzkrise Nicolas Sarkozy
Rais wa Ufaransa,Nicolas SarkozyPicha: AP

Opereshini hii imetokea miaka sabaa baada ya waziri wa mambo ya ndani wakati ule,rais wa sasa Nicolas Sarkozy kuamuru kituo cha wakimbizi kilichokua kikisimamiwa na shirika la kimataifa la msalaba mwekundu cha Sengate kifungwe mnamo mwaka 2002.

Mashirika ya kiutu yanalalamika dhidi ya opereshini ya polisi wanayodai haisaidii kulipatia ufumbuzi tatizo la wakimbizi na badala yake linawafanya wakimbizi kukimbilia katika miji mengine tuu ya mwambao nchini Ufaransa.

"Misitu mengine itaibuka haraka tuu" ameonya mbunge wa eneo hilo wa kutoka chama cha kisoshialisti Jacques Lang.

Katika kambi hiyo ya Calais ,wakimbizi walijipanga nyuma ya mabango yaliyoandikwa kwa kiengereza na kopachtun"Hatuhitaji kulindwa ,tunataka kinga ya ukimbizi na amani.Msitu ndio nyumba yetu."

Mwandishi :Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul-Rahman