1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KAMPALA: Rwanda na Burundi zajiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki

18 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBqa

Rwanda na Burundi leo zimejiujnga rasmi na jumuiya ya Afrika Mashariki. Marais wa jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana leo mjini Kampala Uganda kushuhudia upanuzi wa kanda hiyo ya kiuchumi.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda na Jakaya Kikwete wa Tanzania walikutana mjini Kampala na rais wa Rwanda Paul Kagame na rais wa Burundi, Piere Nkurunziza, kusimamia kujiunga kwa Rwanda na Burundi kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki.

Jumuiya ya Afrika Mashariki sasa ina nchi tano wanachama zikiwemo Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi.

Rwanda na Burundi zilikubaliwa rasmi kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki mnamo mwezi Novemba mwaka jana huku uanachama ukitarajiwa kuanza ramsi Julai mosi mwaka huu. Viongozi wa nchi hizo walitarajiwa pia kuanzisha wimbo wa jumuiya ya Afrika Mashariki na kushuhudia kuapishwa kwa Julius Tangus Rotich raia wa Kenya kama naibu mpya wa katibu mkuu wa jumuiya hiyo.

Kwenye mkutano huo rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alichukua uenyekiti wa jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka kwa rais Mwai Kibaki wa Kenya.