1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KAMPALA:Waasi wa LRA waondoka kusini mwa Sudan

22 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCPg

Waasi wa Lords Resistance Army LRA nchini Uganda wameondoka maeneo mawili walikotakiwa kukusanyika katika eneo la kusini mwa Sudan kwa kuhofia usalama wao.Eneo hilo ndiko ambako mazungumzo ya kutafuta amani na serikali ya Uganda yalikokuwa yakifanyika.

Kwa mujibu wa msemaji wa kundi hilo la LRA waasi hao hawatarejea tena katika meza ya mazungumzo kwenye mji mkuu wa kusini ya Sudan wa Juba.Mpatanishi mkuu Makamu wa Rais Riek Machar kwa upande wake anadai kuwa mazungumzo hayo yalipangwa kuendelea wiki hii.

Makubaliano mapya ya kusitisha vita yaliyofikiwa mwezi Disemba yaliwapa waasi hao hadi mwezi jana kukusanyika katika maeneo mawili ya Owiny-Ki-Bul upande wa Uganda na Ri-Kwangba lililo upande wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Kulingana na msemaji huyo wa LRA wapiganaji wao waliondoka kwenye maeneo hayo na kufumkana.Kwa sasa waasi hao wanajificha kwenye misitu nchini Kongo.

Wajumbe wa LRA wanakataa kurejea katika mazungumzo mjini Juba tangu Rais Omar al Bashir wa Sudan kutisha kuwafurusha kutoka nchini mwake.Mazungumzo hayo ya amani ya Juba yalijaribu kumaliza mapigano ambayo mpaka sasa yamedumu miongo miwili katika eneo la kaskazini mwa Uganda.Mapigano hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuacha wengine milioni 1.7 bila makao.

Makubaliano hayo ya kusitisha vita yanafikia muda wake wa mwisho ifikapo mwisho wa mwezi huu na bado haijulikani lini pande zote mbili watakutana kuuongeza.

Serikali ya Uganda kwa upande wake inashikilia kuwa haitabadilisha sehemu ya mazungumzo kwani LRA kwa upande wao wanasema kuwa hawarudi tena kusini mwa Sudan.