1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni ya uchaguzi mkuu yapamba moto

Oumilkher Hamidou31 Agosti 2009

Matokeo ya uchaguzi wa jana yawazindua wanasiasa wa vyama vikuu mjini Berlin

https://p.dw.com/p/JMXv
Kansela Angela MerkelPicha: AP

Wahafidhina wanaoongozwa na kansela Angela Merkel wanatafakari matokeo ya uchaguzi ulioitishwa jana katika majimbo matatu-Thüringen,Sachsen na Saarland-matokeo yaliyofifiisha matumaini ya kuunda serikali ya muungano pamoja na waliberali,baada ya uchaguzi mkuu wa September 27 ijayo.

Zikisalia wiki nne kabla ya uchaguzi mkuu na muhimu zaidi nchini Ujerumani,chama cha CDU cha kansela Angela Merkel wanatafakari na kusaka mkakati mpya.

Tangu wiki kadhaa sasa taasisi za utafiti wa maoni ya umma zimekua zikiashiria matukio ya uchaguzi mkuu ambayo yangemuwezesha kansela kuachana na muungano pamoja na wasocial Democratic na badala yake kuunda serikali pamoja na chama cha kiliberali cha FDP.

Matokeo mabaya ya uchaguzi wa jana yanazusha suala la kuuliza kama matarajio hayo yatatekelezeka.

Chama cha Christian Democratic cha kansela Angela Merkel kimepoteza kura nyingi katika majimbo mawili ikilinganishwa na mwaka 2004(asilimia 13 ya kura katika jimbo la Saarland na asili mia 11.8 katika jimbo la Thüringen.Hakidhibiti tena wingi wa viti bungeni katika majimbo yote hayo mawili-haya lakini ni kwa mujibu wa matokeo ya muda.

Ingawa kansela Angela Merkel anasalia kuwa kipenzi cha umma,asili mia 62 ya wajerumani wanasema wangependelea aendelee kuwepo madarakani-lakini matumaini ya kushirikiana na waliberali yamefifia.

FDP wamejiimarisha sana kulinganisha na uchaguzi wa mwaka 2004 katika majimbo ya mashariki ya Ujerumani katika wakati ambapo CDU wamekuwa wakiendelea kupoteza sauti katika maeneo hayo naiwe katika chaguzi za mabaraza ya miji,majimbo au hata za ulaya.

Hata hivyo kansela Angela Merkel anasema chama chake ndo mdhamini wa utulivu katika wakati huu wa mizozo:

"Uchaguzi wa jana umedhihirisha kile ambacho Ujerumani inakihitaji,yaani uwiano bayana na madhubuti.Kutokana na hali hiyo,kuanzia sasa na katika kipindi chote cha wiki nne kuelekea uchaguzi mkuu, tutaendelea kusimamia,kutia njiani na kutoa hoja."

Steinmeier / SPD
Mgombea wa SPD,Frank-Walter SteinmeierPicha: AP

Mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo wa Septemba 27 ijayo,waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier wa kutoka chama cha SPD ameyataja matokeo ya uchaguzi wa jana kuwa ni ishara kwamba nchi hii "haiitaki serikali ya muungano wa nyeusi na manjano( yaani CDU/CSU na FDP.)

Katibu mkuu wa chama cha SPD, HUBERTUS HEIL anasema:

"Tumepania kuhakikisha SPD kinazidi kupata nguvu.Lengo letu ni kumuona Frank-Walter Steinmeier akiwa kansela.Anaweza,na hata wapinzani wetu wanajua kama anaweza.Ndio maana tunasema tena tunaweza kuzuwia muungano wa nyeusi na manjano.Na tukifanikiwa,basi kila kitu kitawezekana upande wa SPD hata wadhifa wa kansela."

Kampeni ya uchaguzi mkuu ujao imeanza kuhanikiza.

Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/DPA/AFP

Mhariri:Abdul-Rahman