1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni ya uchaguzi wa Rais nchini Ufaransa yapamba moto.

Mohammed Abdul-Rahman16 Aprili 2007

Ni wiki ya mwisho kabla ya wapiga kura kuamua Jumapili ijayo.

https://p.dw.com/p/CHGF
Mgombea wa chama cha Kisoshalisti Segolene Royal anayewania kuwa mwanamke wa kwanza kuiongoza Ufaransa, akizungukwa na waandishi habari.
Mgombea wa chama cha Kisoshalisti Segolene Royal anayewania kuwa mwanamke wa kwanza kuiongoza Ufaransa, akizungukwa na waandishi habari.Picha: ap

Kampeni ya uchaguzi wa rais nchini Ufaransa imo katika wiki yake ya mwisho, huku mgombea wa chama cha kisoshaisti Segolene Royal akipigania kubakia katika mbio hizo dhidi ya mgombea wa siasa za mrengo wa kulia Nicolas Sarkozy huku akikabiliwa pia na changa moto kutoka kwa mgombea wa tatu Francois Bayrou. Uchaguzi huo wa Rais utafanyika Jumapili ijayo na duru ya pili tarehe 6 mwezi ujao.

Ripoti zinasema hadi sasa takriban theluthi moja ya wapiga kura bado hawajaamua watampigia kura mgombea gani, kukiwa na jumla ya wagombea 12. Mbali na Nicholas Sarkozy anayeekewa matumaini ya kuibuka nafasi ya kwanza katika duru ya mwanzo Jumapili, akifuatiwa na Segolene Royal au Francois Bayrou , mgombe mwengine anayezusha hofu katika mchuano huo ni Kiongozi wa Front National, chama cha msimamo mkali wa bawa la kulia Jean Marie Le Pen.

Utafiti wa maoni unaashiria kwamba ikiwa Bayrou mwenye umri wa miaka 55- atafanikiwa kuingia duru ya pili ana nafasi nzuri ya kumshinda Waziri wa zamani wa ndani Sarkozy katika duru ya pili Mei 6, akitarajia kuungwa mkono na vyama vya mrengo wa shoto. Tayari Waziri mkuu wa zamani , Msoshalisti Michel Rocard na waziri wa zamani Bernard Kouchner wametoa wito wa kuwepo ushirika kati ya chama cha Bayrou Umoja wa democrasia –UDF na kile cha Kisoshalisti kumzuwia Sarkozy ambaye anashutumiwa kuendesha kampeni ya kuwavutia wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia, kutokana na msimamo wake , ikiwa ni pamoja na kuhusu suala la wahamiaji.

Kwa upande wake Sarkozy ameutetea msimamo wake kuhusu wahamiaji, ikiwa ni pamoja na azma yake ya kutaka kuunda wizara mpya ya uhamiaji na nasaba , akisema lengo ni kujenga Ufaransa mpya.Miongoni mwa waliomkosoa ni mchezaji nyota wa timu ya taifa ya kandanda Lilian Thuram, akisema lengo lake hilo ni la hatari na kuiita azma hiyo kuwa ni ubaguzi.

Lakini wakati wito wa ushirika kati ya Royal na Bayrou unaonekana kukaribishwa katika kambi ya Bayrou asiyependelea kuiona Ufaransa inaendelea kuwa katika mgawanyiko kati ya siasa za kulia na shoto na badala yake paweko na nguvu mpya ya bawa la kati na shoto, Bibi Royal bado hajaikaribisha fikra hiyo ya ushirika, akisisitiza anakusudia kuwa “Huru” kama alivyoanza kampeni yake.

Badala yake amewataka wafuasi wa pande zote kumuunga mkono kwa ajili ya haki na amani katika jamii, ili uchaguzi huu usipotee bure kama 2002.

Miaka mitano iliopita, Jean Marie Le Pen alizusha mshtuko alipomshinda mgombea wa chama cha kisoshalisti na waziri mkuu wa zamani Lionel Jospin na kufaulu kuchuana katika duru ya pili na Jacques Chirac aliyeibuka mshindi akiungwa mkono duru ya pili hata na wasoshalisti kumzuwia Le Pen.

Uchaguzi wa Jumapili utakua ni wa kumchagua atakayejaza nafasi inayoachwa na Rais Chirac mwenye umri wa miaka 74, na unaonekana kuwa ni uliojaa shauku kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa robo karne. Chirac aliamua kutogombea tena kipindi cha tatu baada ya mihula miwili.

Wadadisi wanaashiria uwezekano wa kuzuka tena maajabu pengine sawa na yale ya 2002 ,katika uchaguzi huu ambao umeshuhudia idadi kubwa kabisa ya waliojiandikisha kupiga kura. Lakini safari hii pindi yatatokea huenda ikiwa Bibi Royal ataangushwa basi duru ya pili ikawa kati ya Sarkozy na Bayrou au Le Pen…. Ingawa kuna wanaoamini kwamba maajabu yatakayoweza pia kutokea , ni kwamba hatimae kwa mara ya kwanza Ufaransa itaongozwa na mwanamke kama Kiongozi mkuu wa taifa.