1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za Uchaguzi wa bunge na rais zinakamilishwa Kenya

Oumilkheir Hamidou
5 Agosti 2017

Wagombea kiti cha rais Kenya wanahitimisha kampeni zao kabla ya uchaguzi wa Jumanne, Ushindani ni mkali kupita kiasi kati ya wagombea wawili wakuu, rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake wa jadi Raila Odinga.

https://p.dw.com/p/2hk0A
Kenia Wahlkampf | Präsident Uhuru Kenyatta
Picha: Reuters/B. Ratner

Rais Uhuru Kenyatta anashindana kwa mara nyengine tena na kiongozi wa muda mrefu wa upinzani Raila Odinga. Kenyatta ni mtoto wa kiume wa rais wa kwanza wa Kenya, na Odinga ni mtoto wa kiume wa makamu wa kwanza wa rais nchini humo.

Chaguzi za hivi karibuni katika nchi hiyo ambayo ni kitovu cha biashara Afrika Mashariki, zimekuwa zikigubikwa na mabishano makali huku zaidi ya watu elfu moja wakiuwawa kufuatia machafuko ya baada ya uchaguzi mwongo mmoja uliopita.

Waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ni miongoni mwa maelfu ya wanaotazamiwa kusimamia uchaguzi huo.

 Mgombea wa NASA Raila Odinga akiwahutubia wafuasi wake
Mgombea wa NASA Raila Odinga akiwahutubia wafuasi wakePicha: Reuters/J. Keyi

Hofu za kuzuka vurugu zimeenea Kenya

Baadhi katika nchi hiyo yenye wakaazi milioni 44 wamekuwa wakiuhama mji mkuu Nairobi, kwa sababu ya hofu ya kuzuka vurugu huku wengine wengi wakirejea nyumbani kwa ajili ya kupiga kura.

Mateso na mauwaji ya siku za hivi karibuni ya afisa mmoja wa ngazi ya juu wa tume ya uchaguzi aliyekuwa akishughulikia mtambo wa elekroniki wa kupigia kura yamezidisha hofu kuhusu uwezekano wa mori kupaanda wakati wa uchaguzi.

Wasaidizi wa NASA kutoka Marekani na Canada warejeshwa nyumbani

Ndege ya shirika la ndege  la Kenya ikiruka toka uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi
Ndege ya shirika la ndege la Kenya ikiruka toka uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini NairobiPicha: AP

Muungano mkuu wa upinzani NASA umesema raia mmoja wa Marekani na mwengine wa Canada wanaosadia katika kampeni za uchaguzi wa chama hicho, wamechukuliwa toka nyumbani kwao na kuwekwa kizuizini.

James Orengo, mwanachama mashuhuri wa muungano wa National Super Alliance-NASA amesema kamatakamata hiyo imetokea takriban wakati mmoja na kuvamiwa kituo chao cha kuhesabu kura, na polisi waliokuwa na silaha na ambao walificha nyuso zao, polisi waaliowatisha wafanyakazi wa kituo hicho na kuondoka na vifaa kadhaa.

Afisa wa polisi amesema maafisa wa uhamiaji wanawashikilia raia hao wawili wa kigeni, Mmarekani na Mcanada kataka uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta International Aiport mjini Nairobi. Afisa huyo ameliambia hayo shirika la habari la AP akisisitiza hataki jina lake litajwe kwa kuwa haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari.

Hata hivyo ubalozi wa Marekani nchini Kenya umesema kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa raia hao wako salama na kuwa wako njiani kurejea nyumbani. Ubalozi huo umeongeza kuwa wamekuwa wakiwasiliana na maafisa wa Canada na maafisa wa serikali ya Kenya kuhusu kisa hicho.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP

Mhariri: John Juma