1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampuni la Arcandor lajitangaza muflis

Oumilkher Hamidou10 Juni 2009

"Fursa ya kuchipuka upya" anasema kansela Angela Merkel

https://p.dw.com/p/I6jd
Kansela Angela MerkelPicha: AP

Kampuni la Ujerumani la shughuli za kibiashara na Utalii -ARCANDOR,limeachana na juhudi zake za kuomba msaada wa fedha za serikali na badala yake limejitangaza muflis.Kabla ya hapo maelfu ya wafanyakazi wa Arcandor waliitisha maandamano kadhaa,mikutano kadhaa ya hadhara na kukusanya saini za watu ili kuitanabahisha serikali kuu ya mjini Berlin ikubali kulisaidia kifedha kampuni hilo.Lakini serikali ilipinga maombi hayo.Kansela Angela Merkel anahisi tangazo la muflis ni fursa ya kuchipuka upya Arcandor.

Mjini Berlin hakuna aliyeshtuka alipopata habari kwamba kampuni la Anrcandor limejitangaza muflis."Nimepata habari" amesema kansela Angela Merkel na kuongeza kusema kwamba hatua hiyo italifungulia njia mpya kampuni hilo.Kuna uwezekano kwa mfano wa kuchanganyika na kampuni kubwa la maduka la Metro.Kansela Angela Merkel anasema:

"waziri wa uchumi wa serikali kuu ataanza haraka kuzungumza pamoja pia na wawakilishi wa wafanyakazi wa Arcandor,kwasababu serikali kuu ya Ujerumani ina hamu kubwa ya kutaka kusaidia.Daima tumekua tukisema tangazo la kufilisika linaweza kulifungulia njia ya kuchipuka upya kampuni hili,kulipatia matumaini mema na serikali itasaidia kwa kadri itakavyoweza.Kwa maoni yetu lakini, ahadi zilizotolewa na wamiliki mali na waiya kuliokoa kampuni la Arcandor zilikua haba.Tunabidi pia tuzingatie fedha za walipa kodi.Kwa hivyo hii ni hatua ambayo haiepukiki,lakini ni hatua inayofungua fursa ambazo lazma zitumiwe kuambatana na muongozo wa sheria za Ujerumani."

Kabla ya hapo serikali kuu ya Ujerumani ilikataa kulipatia msaada kampuni hilo.Wamiliki mali walitakiwa wawajibike zaidi na kuchangia msaada mkubwa zaidi kuliko ule walioahidi kutoa-alishadidia waziri wa uchumi Karl-Theodor zu Guttenberg:

"Kuna orodha ya vifungu kumi vinavyozungumzia masharti yaliyowekwa.Imetajwa katika orodha hiyo kwamba mchango wa wamiliki mali na waiya unabidi uongozwe.Tunahitaji waraka wa maridhiano pamoja na benki unaoonyesha kwamba katika kipindi kizima cha juhudi za kuliokoa kampuni hilo,benki zitajizuwia na kwamba hakuna madai yoyote ya mabilioni ya fedha yatakayotolewa msimu wa mapukutiko utakapowadia."

Sio tuu vyama ndugu vya CDU/CSU,bali hata katika chama cha SPD,kuna watu waliokua wakisita sita kuhusiana na suala la Arcandor kupatiwa msaada wa serikali.Hata hivyo naibu kansela,waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinemeier amesikitika baada ya kushindwa juhudi za kulinusuru kampuni hilo.Anasema angali anaamini madai ya muflis yangeweza kuepukwa na kuiongeza tunanukuu:"Tutaendelea kuwaunga mkono wafanyakazi na kupigania masilahi yao.

Mwandishi:Marx,Bettina(DW Berlin)/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul Rahman