1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampuni za Marekani zapinga vikwazo dhidi ya Venezuela

Zainab Aziz
10 Agosti 2017

Marekani yawawekea vikwazo maafisa wengine wanane wa bunge maalum la katiba la nchini Venezuela. Hadi sasa idadi ya wawakilishi wa serikali waliowekewa vikwazo imefikia watu 30. 

https://p.dw.com/p/2hzJK
Venezuela Krise - Präsident Maduro während seiner TV-Ansprache
Picha: Reuters/Miraflores Palace

Hata baada ya serikali ya Marekani kuviweka vikwazo hivyo dhidi ya wawakilishi wa bunge maalum lenye nguvu kubwa nchini Venezuela vikwazo hivyo vya kifedha huenda visianze kufanya kazi  mara moja kutokana na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wa mafuta nchini Marekani ambao wanasema vikwazo vinavyolenga sekta ya mafuta nchini Venezuela ambayo ndio inashikilia nafasi ya tatu kwa waingizaji wa mafuta nchini Marekani vitasababisha waajiri kuwaachisha kazi wafanyakazi wao na pia vitasababisha kuongezeka kwa bei ya gesi nchini humo.

Kampuni zaidi ya 20 za Marekani ikiwa ni pamoja na Chevron, Valero, Citgo na Phillips 66 kwa sasa zinafanya biashara ya kusafisha mafuta kutoka Venezuela. Nyingi ya kampuni hizo zinafanya shughuli zake katika eneo la Ghuba.  Kwa mujibu wa taarifa ya wasimamizi wa Nishati nchini Marekani  kampuni hizo zitalazimika kubadili muundo wa mashine zake za kusafishia mafuta kwa kuwa ziliundwa kwa ajili ya kusafisha mafuta mazito kutoka Venezuela na zoezi hilo litakuwa ni la gharama kubwa. 

Venezuela Ölfässer von Venoco
Mapipa ya mafuta ambayo hayajasafishwa ya Venezuela Picha: Getty Images/AFP/M. Gutierrez

Waziri wa mambo ya nje wa Venezuela Jorge Arrenza amepinga vikali vikwazo hivyo vipya vya Marekani dhidi ya wanachama hao wanane wa bunge maalum la katiba. Waziri huyo wa mambo ya nje amesema hatua hii inaonyesha jinsi gani ambavyo Marekani,haiheshimu kanuni yoyote ya msingi na pia haikufuata misingi ya sheria za kimataifa.

Vikwazo hivyo vinawalenga maafisa wanaoitumikia serikali kwa sasa na wale wa zamani ambao wanaiunga mkono hatua ya serikali ya rais Nicolas Maduro ya kuanzisha bunge maalum ambalo limepewa uwezo wa kuiandika upya katiba ya Venezuela. Wizara ya fedha ya Marekani ilichukua hatua isiyo ya kawaida ya kuidhinisha hatua ya kufungia mali yoyote anayoweza kuwa nayo rais Maduro nchini Marekani na vilevile kuwazuia Wamarekani kufanya biashara na Venezuela. Vikwazo hivyo vipya vinamlenga pia Adan Chavez, ambaye ni ndugu wa aliyekuwa rais wa Venezuela marehemu Hugo Chavez, aliyejulikana kwa kuanzisha itikadi ya Kimarxi kwenye miaka ya 70.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga