1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanisa Katoliki lalegeza kamba matumizi ya kondom

Saumu Ramadhani Yusuf22 Novemba 2010

Papa Benedikto wa 16 asema kondom zinaweza kutumika pale inapolazimu

https://p.dw.com/p/QF7W
Picha: AP

Kiongozi wa kanisa Katoliki ameushangaza ulimwengu kwa hatua yake ya kubadili msimamo kuelekea matumizi ya mipira ya kinga (Condom). Msimamo huo wa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani umeelezewa katika kitabu chake kipya kinachotazamiwa kuchapishwa kesho, Jumanne, ambapo ameeleza kwamba kutumia Kondom baadhi ya wakati kunakubalika ili kuzuia kueneza magonjwa.

Wakatoliki wenye msimamo wa wastani, wanaharakati wanaojihusisha na masuala ya maradhi ya Ukimwi pamoja na maafisa wa afya wameupongeza msimamo wa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani, wakisema ni ushindi mkubwa na hatua kubwa ya kuelekea mbele katika kutambua kwamba matumizi ya mipira ya Kondom yanaweza kuchukua nafasi kubwa katika kupunguza athari zaidi ya virusi vya HIV siku za baadae.

Katika kitabu chake kipya, kinachoitwa nuru ya ulimwengu, papa ameeleza kwa maneno yake akitoa mfano kwa kusema matumizi ya Kondom kwa makahaba ni hatua ya kwanza kuelekea katika kuwabadilisha kimaadili watu hao, ingawa Kondomu sio njia ya kweli ya kupambana na maambukizi ya virusi vya HIV.

Papst Benedikt XVI mit irischen Bischöfen bei Gesprächen im Vatikan
Papa Benedict XVI, na Maaskofu kutoka Ireland,Picha: AP

Hata hivyo, katika kitabu hicho ambacho kimeandikwa kwa Kijerumani, kifaransa na kiingereza kinazungumzia juu ya makahaba wa kiume, ingawa katika kipande cha maneno yaliyotafsiriwa kwa Kitaliana katika gazeti la Vatican kinazungumzia kuhusu makahaba wa kike.

Pamoja na hayo, lakini wanaharakati mbali mbali duniani wameusifu msimamo wa kanisa Katoliki, na hasa ikizingatiwa kwamba viongozi wa dini mbali mbali wanapinga matumizi ya Kondom nje ya ndoa. Peter Seewald, mwandishi wa habari wa kikatoliki kutoka Ujerumani, ambaye mahojiano yake na Papa ndiyo yaliyotumiwa kuandika kitabu hicho kipya cha Papa, anasema msimamo huo wa Papa unabidi kupongezwa kwani sio hatua ya kawaida katika historia ya kanisa hilo.

Kanisa Katoliki limekuwa likisema kwa miongo kadhaa kwamba kondomu sio sehemu ya kuleta suluhisho katika vita dhidi ya maradhi ya Ukimwi, ingawa hakujakuweko msimamo kuhusiana na jambo hilo katika maandiko ya Vatikani. Itakumbukwa kwamba mwaka jana kiongozi huyo wa Kanisa Katolki alizusha hisia kali miongoni mwa walimwengu alipokuwa katika ziara barani Afrika na kusema kwamba Kondomu hazipaswi kutumiwa kwa sababu zinaweza kuzidisha maambukizi ya virusi vya HIV na maradhi ya Ukimwi.

5 Jahre Papst Benedikt XVI Afrika 2009 Flash-Galerie
Papa alipokuwa Cameroon mwaka janaPicha: AP

Hata hivyo, viongozi wa kidini kutoka makanisa mengine duniani hawakubaliani na msimamo wa kuridhia matumizi ya Kondom kwa kila anayetaka kufanya hivyo, bali yanaruhusiwa kwa wanandoa tu.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, pia ameusifu msimamo wa Papa ambaye katika kitabu chake pia amepinga ndoa za jinsia moja, ingawa suala hilo limewakasirisha sana wanaharakati wa kutetea haki za mashoga na wasagaji duniani.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri Othman Miraji