1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uongozi wa Merkel ni muhimu kwa Ulaya

22 Novemba 2015

Miaka kumi tangu alipokabidhiwa kwa mara ya kwanza hatamu za uongozi,kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesalia kuwa mshika bendera asiyebishika barani ulaya licha ya mizozo,na licha ya kupungua umashuhuri wake .

https://p.dw.com/p/1HAE1
Angela Merkel alipochaguliwa upya mwaka 2009Picha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Miaka kumi tangu alipokabidhiwa kwa mara ya kwanza hatamu za uongozi,kansela wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Angela Merkel amesalia kuwa mshika bendera asiyebishika barani ulaya licha ya kukabiliana na mizozo ya kila aina,na licha ya kupungua kidogo umashuhuri wake nchini.

Akitanguliza mbele maadili ya Ulaya,Agela Merkel aliamua msimu wa kiangazi mwaka huu kuwakaribisha mikono miwili wakimbizi nchini Ujerumani.Kabla ya hapo alichangia kuimarisha mshikamano katika kanda ya Euro wakati Ugiriki ilipobanwa na mgogoro wa fedha na kutayarisha jibu la nchi za Ulaya kwa mzozo wa Ukraine.

Nguvu za kiuchumi za Ujerumani,zikichanganyika na udhaifu wa washirika wake ndani ya Umoja wa ulaya umemfanya ageuke "malkia wa ulaya" na hilo,licha ya kwamba wagiriki waliwahi wakati mmoja kuichoma moto picha yake na kwamba katika nchi za Ulaya ya mashariki ,anabebeshwa jukumu la mikururo ya wakimbizi.

Kutokana na suala hilo hasa ndio maana umashuhuri wake unalega lega kidogo nchini katika wakati ambapo Umoja wa Ulaya unahitaji kiongozi imara.

"Kwakua Umoja wa ulaya umedhihirika unashindwa kuzuwia mizozo,limekuwa jukumu la Merkel kuzuwia mpasuko ndani ya Umoja wa Ulaya"anachambua Judy Dempsy,mwanachama wa shirika lisilomilikiwa na serikali Carnegie Europe,mhariri wa kitabu kinachomhusu kansela Angela Merkel."Si kazi ya kumezewa mate,imejaa vishindo"ameandika.

Angela Merkel amempita Barack Obama katika orodha ya viongozi wenmye ushawishi ulimwenguni

Ushahidi wa umuhimu wake,Merkel anakamata nafasi ya pili nyuma ya Vladimir Putin katika orodha ya viongozi wenye ushawishi mkubwa ulimwenguni iliyochapishwa hivi karibuni na jarida la Forbes.Amempita kwa namna hiyo rais Barack Obama wa Marekani katika orodha hiyo ya Forbes.Na jarida la The Economist limemtaja katika toleo lake la hivi punde kuwa "kiongozi asiyeweza kukosekana barani Ulaya."

Jacob Zuma Südafrika mit Angela Merkel Berlin Deutschland
Kansela Merkel alipomkaribisha rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma mjini BerlinPicha: Getty Images/S.Gallup

"Miaka hii ya nyuma ameshikilia nafasi muhimu katika kuipatia ufumbuzi mizozo na kusaidia kusawazisha hali za kutatanisha kabisa"ameeleza Janis Emmanouillidis,wa taasisi ya siasa za Ulaya-EPC.

Hata hivyo bibi huyo aliyetokea Ujerumani mashariki ya zamani,ameanzia jukumu lake la kuiongoza Ujerumani mwaka 2005 bila ya kishindo,akirejesha hatua baada ya hatua uhusiano pamoja na Marekani,uliodhoofika baada ya Berlin na Paris kupinga uvamizi wa Marekani nchini Iraq mwaka 2003.

Akiwa na shahada ya uzamili ya fizikia,Merkel huonekana kufuata zaidi utaratibu wa kisayansi katika kuipatia ufumbuzi mizozo,kwa kusubiri kwanza ,kama ilivyoshuhudiwa wakati wa mzozo wa madeni katika kanda ya Euro.

Na msimamo mkali unaotetewa na Ujerumani,inayodai hatua za kufunga mkaja katika nchi zinazozongwa na m gogoro wa fedha,umechangia kuifanya nchi hii isipendwe na hasa na Ugiriki ambako jinamizi la kuvamiwa na wanazi bado halijatoweka.

Lakini yeye pia ndie aliyefanya kila la kufanya msimu wa kiangazi mwaka huu ili Ugiriki iendelee kuwa mwanachama wa kanda ya Euro.

Mpaka Vladimir Putin anamheshimu Angela Merkel

Kuhusu Ukraine,katika wakati ambapo Ulaya nzima iliachwa kando,alikuwa kwa mara nyengine Merkel aliyekwenda Minsk pamoja na rais wa Ufaransa Francois Hollande kuzungumzia mpango wa kuweka chini silaha,februari mwaka huu.

Berlin Bundeskanzleramt Seehofer Gabriel Merkel Koalition
Kansela Angela Merkel,baada ya mazungumzo pamoja na washirika wa serikali ya muungano,Horst Seehofer wa chama cha CSU na Sigmar Gabriel wa SPD kuhusu mzozo wa waakimbiziPicha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Inasemekana pia kwamba kansela Merkel tu ndie kiongozi wa Ulaya anaeheshimiwa na rais wa Urusi Vladimir Putin.

Mzozo wa wakimbizi umempatia nafasi nyengine ya kudhihirisha cheo chake cha uongozi barani Ulaya;kutokana na wimbi la wakimbizi na katika wakati ambapo idadi kubwa ya viongozi wa Ulaya wanaelezea wasi wasi wao kutokana na kuibuka makundi ya siasa kali,kansela Merkel aliwashangaza wote alipowafungulia wakimbizi milango ya Ujerumani.

Lakini tangazo hilo limeidhoofisha kidogo msimamo wake barani Ulaya.Mataifa ya Ulaya ya kati na Mashariki yanamlaumu kuwapa moyo wakimbizi wazidi kuingia katika nchi zao wakiwa njiani kuelekea Ujerumani.

Hali hiyo imefika hadi ya kuathiri umashuhuri wa kiongozi huyo wa serikali kuu ya Ujerumani ambae kawaida daima alikuwa akiongoza katika orodha ya wanasiasa wanaopendwa sana na wananchi humu nchini.Wajerumani wanahofia jumla ya wakimbizi milioni moja wataingia humu nchini mwaka huu.

Uamuzi wake wa ghafla kuhusu wakimbizi unakumbusha mtihani mwengine uliotokea mwaka 2011 baada ya ajali katika mtambo wa nuklea wa Fukushima nchini Japan na kupelekea kansela Merkel kutangaza Ujerumani itaachana na nishati ya nuklea hatua baada ya hatua.

"Hata kama kuna wanaombisha,lakini Merkel anasalia kuwa malkia wa Ulaya" wanakubaliana wadadisi barani Ulaya."Hakuna lolote muhimu linaloweza kutendeka bila ya ridhaa ya Ujerumani,Yeyote anaeongoza serikali Berlin,atakuwa na jukumu pia la kuongoza barani Ulaya" wanasema wadadisi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu