1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel ahutubia bungeni

Oumilkher Hamidou26 Machi 2009

NATO ijiandae kwa changamoto za aina mpya

https://p.dw.com/p/HKFa
Kansela wa Ujerumani bibi Angela MerkelPicha: AP


Kansela Angela Merkel amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa dhati kati ya Urusi na jumuia ya kujihami ya NATo.Matamshi hayo ameyaatoa kansela mbele ya wabunge wa shirikisho mjini Berlin.


Katika hotuba yake mbele ya bunge la shirikisho,Bundestag,kabla ya mkutano wa kilele wa jumuia hiyo ya NATO kuitishwa,kansela Angela Merkel amesifu mchango wa NATO.Amekumbusha hata hivyo watu wasitulie kutokana na ufanisi wa miaka 60 iliyopita ,"kuna mengi yanayobidi kutekelezwa kuelekea miaka ijayo."


Kansela Merkel amesema


"Katika mkutano wa kilele tunabidi kwa hivyo tutathmini upya mkakati wetu ili kuweka wazi kabisa kwamba NATO haijiachii tuu kuridhika na yaliyotokea miaka 60 iliyopita,bali iko tayari pia kukabiliana na mkondo mpya wa siku za mbele."


Kansela Angela Merkel ameonya hata hivyo dhidi ya kugeuzwa jumuia hiyo kua polisi ya dunia.Licha ya juhudi zake za kijeshi nje ya mipaka ya nchi wanachama wa NATO,jukumu kubwa la jumuia hiyo ,anasema kansela Angela Merkel,ni kudhamini usalama wa mataifa wanachama.


Wiki moja kabla ya mkutano wa kilele wa NATO utakao adhimisha miaka 60 tangu jumuia hiyo ilipoundwa,kansela Angela Merkel amezungumzia matarajio ya Georgia na Ukraine ya kujiunga na NATO,akisema hata hivyo mipango ya kupanuliwa jumuia hiyo inabidi iwe na vikomo.Kansela Angela Merkel ametetea umuhimu wa kushirikiana kwa dhati na Urusi katika masuala ya usalama na kuitolea mwito Urusi itoe ishara ya kurejesha hali ya kuaminiana pamoja na jumuia ya kujihami ya NATO.


Kansela Angela Merkel amesema atayazusha masuala ya usalama atakapokutana na rais Dmitri Medvedev wa Urusi jumanne ijayo mjini Berlin.


Kuhusu kuwajibika vikosi vya Ujerumani nchini  Afghanistan kansela Angela Merkel ameweka wazi kabisa,kwasasa halizuki suala la kuongezwa wanajeshi wa Bundeswehr nchini humo.


Kansela Angela Merkel amekumbusha bunge la shirikisho limeidhinisha mwaka jana kutumwa wanajeshi elfu moja zaidi nchini Afghanistan na kwamba Ujerumani inachangia pia katika kuijenga upya Afghanistan na kuwapatia mafunzo askari polisi.