1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uwiano na tofauti pia ziko

10 Machi 2015

Na sasa tunaelekea Japan ambako kansela Angela Merkel wa Ujerumani akikamilisha ziara yake hii leo ametetea umuhimu wa kutiwa saini makubaliano ya biashara huru kati ya Japan na nchi za Umoja wa ulaya.

https://p.dw.com/p/1Eo1z
Kansela Angela Merkel akikitembelea kiwanda cha magari ya Mitsubishi huko KawasakiPicha: AFP/Getty Images/T. Kitamura

Ziara ya kansela Angela Merkel imedumu siku mbili.Jana alikuwa na mazungumzo pamoja na waziri mkuu Shinzo Abe na mfalme Akihito.Hii leo mnamo siku ya mwisho ya ziara hiyo,kansela Angela Merkel alikitembelea kiwanda cha kutengeneza malori chapa Mitsubishi Fuso katika mji wa Kawasaki-ulioko karibu na Tokyo.Huko kansela Angela Merkel aligusia suala la usafi wa mazingira akisema " tofauti japo kidogo katika vipimo vya moshi unaotoka ndani ya magari inamaanisha kazi nyingi katika kuyachunguza magari".Na hiyo ndio sababu anasema kansela Angela Merkel makubaliano ya biashara huru ni muhimu na yanaweza kuleta ufanisi.

Kampuni la Mitsubishi Fuso limeundwa kutokana na ushirikiano kati ya kampuni la Ujerumani Daimler AG na lile la Japan Mitsubishi Cooporation ambapo mchango wa Ujerumani unafikia asili mia 90.Likiwa na wafanyakazi 11000 kampuni hilo linaangaliwa kuwa kubwa kabisa miongoni mwa makampuni ya Ujerumani nchini Japan.

Kuna mengi yanayolingana,lakini pia kuna tofauti

Kabla ya kuondoka mjini Tokyo kurejea Berlin kansela Angela Merkel amezungumzia maarifa aliyoyapata kutokana na ziara yake hiyo fupi nchini Japan akisema "kuna mengi yanayolingana , kuna tofauti pia lakini kuna sababu nzuri pia za kuimarisha uhusiano kati ya Ujerumani na Japan na sio tu katika sekta ya kiuchumi,bali pia katika masuala ya usalama na mabadiliko katika hali ya wakaazi.Kansela Angela Merkel anaendelea kusema:"Mada iliyokamata nafasi muhimu katika ziara hii ni mabadiliko ya hali ya wakaazi.Suala hili linaweka wazi kabisa umuhimu wa kuwajibishwa akinamama.."Mkondo huu tunaushuhudia pia nchini Ujerumani."

Japan Angela Merkel mit Premierminister Shinzo Abe in Tokio
Kansela Angela Merkel na waziri mkuu Shinzo AbePicha: Reuters/S. Kambayashi

Usawa wa jinsia ndio mada muhimu katika zamu ya Ujerumani kama mwenyekiti wa G-7

Kabla ya hapo kansela Angela Merkel alikutana na akinamama wanaoshikilia nyadhifa za juu.

Japan Angela Merkel besichtigt ein Mitsubishi-Werk in Kawasaki
Kanasela Merkel akizungumza na watumishi wa kiwanda cha MitsubishiPicha: Reuters/T. Peter

Kama ilivyokuwa wakati wa ziara yake mjini Washington,kansela Angela Merkel aliarifiwa kuhusu matatizo wanayokabiliana nayo akinamama wanaoshikilia nyadhifa za juu.Suala la kuhimiza usawa wa jinsia na akinamama kujitegemea ni miongoni mwa mada kuu za Ujerumani kama mwenyekiti wa kundi la mataifa sabaa tajiri kiviwanda duniani-G7.Mwezi Juni mwaka huu kansela Angela Merkel atawakaribisha viongozi wa taifa na serikali kutoka mataifa hayo sabaa ambayo ni pamoja na Marekani,Canada,Japan,Italia,Ufaransa,na Uengereza katika kasri la Elmau katika jimbo la kusini la Bavaria.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/Afp

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman