1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel akutana na rais Sarkozy mjini Paris

Oumilkher Hamidou11 Juni 2009

Mazungumzo ya kusawazisha misimamo kabla ya mkutano wa baraza la ulaya wiki ijayo

https://p.dw.com/p/I7ZZ
Rais Sarkozy na kansela Angela MerkelPicha: picture-alliance/ dpa

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekutana na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa hii leo mjini Paris kwa mazungumzo yaliyolenga kusawazisha misimamo yao kabla ya mkutano wa baraza la Ulaya June 18 hadi 19 ijayo.

Mada kadhaa muhimu zilijadiliwa na viongozi hao wawili katika mkutano huo unaotajwa kua "mashauriano ya kawaida kati ya madola haya mawili."Mada hizo ni pamoja na hali ya kiuchumi ulimwenguni,uchaguzi wa bunge la Ulaya na matokeo yake hadi kufikia suala la kiongozi wa upande wa upinzani nchini Burma,Aung San Suu Kyi.

Kansela Angela Merkel na mwenyeji wake rais Nicolas Sarkozy,wakipata moyo kutokana na vyama vyao vya mrengo wa kulia kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa bunge jumapili iliyopita,wameelezea uungaji mkono wao usio na "walakin" kwa mwenyekiti wa sasa wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya aendelee na wadhifa wake.

Merkel empfängt Barroso
Kansela Merkel na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya BarrosoPicha: picture-alliance/ dpa

"Tunamuunga mkono Barroso bila ya walakini" amesema hayo rais Sarkozy wakati wa mkutano wa waandishi habari pamoja na kansela Ángela Merkel.

Tunataka lakini aelezee msimamo wake kikamilifu,azungumzie majukumu yake kwa Ulaya, majukumu yanayowalinda raia wa Ulaya.

Kansela Angela Merkel amesema :

"Hiyo ndio maana Ufaransa na Ujerumani zinamuunga mkono Jose Manuel Barroso.Na ndio maana tutaendeleza mkakati wa maana kwa namna ambayo ikiwa bunge litapendelea ,basi mwenyekiti wa halmashauri kuu anaweza kuchaguliwa mwezi ujao wa July."

Kansela Angela Merkel na rais Sarkozy wanataka mkutano ujao wa baraza la Ulaya ufafanue masuala yote yaliyopelekea kukwama utaratibu wa kuidhinishwa mkataba wa Lisbone.

Ufaransa na Ujerumani zinashikilia pia maamuzi yaliyofikiwa wakati wa mkutano wa kilele wa G-20 ,April pili mwaka huu,yatekelezwe.Kansela Angela Merkel na rais Nicolas Sarkozy wanataka shughuli za kusimamia masoko ya hisa ziimarishwe.Wanapinga fikra ya kutoa ridhaa ziada.Kwa upande huo kiansela Angela Merkel anasema tunanukuu:"Mada kuu itakayojadiliwa wiki ijayo katika mkutano wa baraza la ulaya itahusu bila ya shaka,maendeleo yanayobidi kufikiwa katika kusimamiwa shughuli za masoko ya fedha"-Mwisho wa kumnukuu kansela Angela Merkel aliyehimiza Ulaya iwe mshika bendera wa kanuni za masoko ya fedha.

Kansela Angela Merkel na rais Sarkozy wameisifu ripoti ya mwenyekiti wa zamani wa shirika la fedha la kimataifa IMF,Jacques de Larosière,aliyoiandaa kwa niaba ya mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya,Barroso."Ujerumani na Ufaransa zitahakikisha ripoti hiyo inatekelezwa-amesema kansela Merkel.

Kuhusu Myanmar,viongozi hao wawili wamelaani msimamo wa utawala wa kijeshi dhidi ya mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel Aung San Suu Kyi.

Kansela Angela Merkel na rais Nicolas Sarkozy wamesema wameingia na wasi wasi kuhusu hali ya bibi huyo mpole mwenye umri wa miaka 63.Wamezitaka China na India ziingilie kati,kabla ya hukumu dhidi yake kutangazwa siku chache zijazo.


Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman