1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel akutana na waziri mkuu wa Ethiopia.

4 Oktoba 2007

Katika kituo cha kwanza cha ziara yake barani Afrika, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel leo amefanya mazungumzo na waziri mkuu wa Ethiopia bwana Meles Zenawi mjini Addis Ababa.

https://p.dw.com/p/C788
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: AP

Kwenye mazungumzo hayo Kansela Merkel alimtaka mwenyeji wake waziri mkuu Zenawi afanye juhudi zaidi katika utekelezaji wa haki za binadamu.

Bibi Merkel amesema ,sera za uwazi, kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari ni pembejeo zinazochangia katika kuleta maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wake waziri mkuu wa Ethiopia bwana Zenawi amesema kuwa nchi yake inafanya juhudi kuelekea kwenye mgawanyo wa madaraka. Lakini bwana Zenawi ameeleza kuwa ni vigumu kwa Ethiopia kufikia shabaha ya demokrasia katika msingi wa mtazamo wa nchi za magharibi.

Kansela wa Ujerumani bibi Merkel pia amesisitiza umuhimu wa bara la Ulaya katika kushirikiana na nchi za Afrika. Amesema bara la Ulaya linapaswa kufanya juhudi zaidi.

Kansela Merkel anafanya ziara barani Afrika kuashiria dhamira ya Ujerumani na nchi tajiri duniani, katika kutimiza ahadi zilizotoa juu ya kushirikiana na bara hilo katika juhudi zake za kupambana na umasikini.

Hatahivyo Kansela Merkel amesema pana haja ya kuweka miundombinu inayostahili ili kufanikisha juhudi hizo.Kabla ya kuondoka Ethiopia, kiongozi huyo wa Ujerumani atatoa hotuba kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika.

Pia anatarajiwa kukutana na rais wa tume ya Umoja wa Afrika bwana Alpha Oumar Konare ili kujadili mpango wa kupeleka jeshi la pamoja na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kulinda amani katika jimbo la Darfur.

Baada ya ziara yake nchini Ethiopia bibi Merkel atawasili nchini Afrika Kusini ambapo atatumia muda wa siku tatu wa mazungumzo na mwenyeji wake rais Thabo Mbeki na kukutana, na kiongozi jarabati wa nchi hiyo mzee Nelson Mandela.Kansela Merkel pia atakutana na kiongozi wa upinzani.

Kansela Merkel atamaliza ziara ya bara la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara kwa kuitembelea Liberia.