1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel atetea mpango wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Umoja wa Ulaya

Mohamed Dahman8 Machi 2007

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amewataka viongozi wa Umoja wa Ulaya leo hii kuharakisha juhudi za dunia kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kuweka malengo makubwa na kukataa wasi wasi kutoka makampuni juu ya gharama kubwa katika kufikia malengo hayo.

https://p.dw.com/p/CHIc
Kansela Angela Merkel akiwa mjini Brussels Ubelgiji kabla ya kufunguliwa kwa mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya tarehe 8 Machi 2007.
Kansela Angela Merkel akiwa mjini Brussels Ubelgiji kabla ya kufunguliwa kwa mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya tarehe 8 Machi 2007.Picha: AP

Viongozi kutoka mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya wanatazamiwa kuhudhuria mkutano huo wa viongozi kuunga mkono malengo ya kupunguza utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira kunakolaumiwa kusababisha ongezeko la ujoto duniani kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2020 kulinganishwa na viwango vya mwaka 1990 na kuachana na asilimia 30 iwapo nchi nyengine kuu zinazochangia kuchafuwa mazingira zitajiunga na mpango huo.

Merkel ambaye ni rais wa sasa wa Umoja wa Ulaya anakabiliwa na kazi pevu kuweka malengo ya kujifunga na kufanya nishati zinazoweza kutumiwa tena kama vile mwanga wa jua na upepo inayofanya asilimia 20 ya matumizi ya nishati wakati nchi nyingi zikiwa hazishtushwi na gharama halisi ya kutekelezwa hayo.

Katika masuala ya kujifunga kimajukumu juu ya nishati zinazoweza kutumiwa upya Ernest Antoine Seilliere Mfaransa ambaye ndie mwenyekiti wa kundi la kupiga debe la Biashara Ulaya ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa viongozi kwamba hakuna mtu mwenye wazo juu ya jinsi gharama zitakyokuwa katika kutimiza malengo hayo.

Merkel amemjibu kwa kusema kwamba malengo ya kujifunga yataweka mfumo wa wazi wa sheria ambao yeye pamoja na viongozi wengine wa biashara walidai na amesema kwamba itakuwa gharama kubwa zaidi kuchelewesha kuchukuliwa kwa hatua za kupiga vita uchafuzi wa mazingira.

Merkel ambaye pia ni mwenyekiti wa kundi la mataifa manane yenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani amesema anataka Umoja wa Ulaya kuwa wa kwanza kuweka mfano juu ya mashaka yaliopo kwa mabadiliko ya hali ya hewa.Nchi kutoka kundi la mataifa manane pamoja na Brazil,China,India, Mexico na Afrika Kusini zinatazamiwa kukutana nchini Ujerumani hapo mwezi wa Juni.

Merkel amesema tatizo hasa la mabadiliko ya hali ya hewa halitotatuliwa na Ulaya pekee kutokana na Ulaya kutowa kama asilimia 15 ya gesi zenye kuathiri mazingira duniani.

Katika mkutano huo Merkel ameandamana na mawaziri wakuu 16 wa majimbo ya Ujerumani.

Halmshauri ya Umoja wa Ulaya ambayo ilirasimu mapendekezo ya kuwa na sera ya pamoja ya nishati ya Umoja wa Ulaya inasema malengo ya kupunguza utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira yasio ya kushurutisha hayawezi kufanya kazi.Nishati zinazoweza kutumika tena hufanya pungufu ya asilimia saba ya nishati ya jumla ya Umoja wa Ulaya nje ya lengo la hiari kufika asilimia 12 ifikapo mwaka 2010.

Mawaziri Wakuu wa Denmark,Sweden na Luxemburg wote wamejitokeza kwa nguvu kuunga mkono shinikizo la Ujerumani la kuwa na malengo ya kujifunga kupunguza gesi zinaziathiri mazingira kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa viongozi lakini mapendekezo yake yamezusha tafshani katika serikali kadhaa za nchi za Umoja wa Ulaya.