1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel azuru Saudi Arabia

Josephat Nyiro Charo26 Mei 2010

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel yuko nchini Saudi Arabia, kituo chake cha pili cha ziara yake ya nchi za Ghuba. Anatokea Abu Dhabi ambako alizataka nchi za Ghuba kusaidia kuishinikiza Iran na mpango wake wa nyuklia

https://p.dw.com/p/NX9a
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kulia) na mfalme Abdullah wa Saudi ArabiaPicha: AP

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema baada ya kukutana leo na mfalme Abdullah wa Saudi Arabia mjini Jeddah kwamba kiongozi huyo ameitaka Ulaya iongeze juhudi zake katika mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.

"Mfalme Abdullah amevunjika moyo sana na jinsi mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati yanavyokwenda," amesema kansela Merkel baada ya kukutana na mfalme Abdullah huko Jeddah.

Mfalme huyo amependekeza njia kadhaa zinazoweza kuharakisha mchakato mzima wa kutafuta amani na kuihimiza Ujerumani na Umoja wa Ulaya zishirikiane kwa karibu zaidi na Marekani katika kufanikisha mazungumzo ya amani.

Kuhusu Iran kansela Merkel amesema mfalme Abdullah anaunga mkono juhudi za kuishawishi Urusi na China zikubali wazo la vikwazo vipya dhidi ya Iran vinavyolenga kuishinikiza nchi hiyo ieleze wazi malengo ya mpango wake wa nyuklia uliozusha utata. Saudi Arabia itatumia uhusinao wake wa kidiplomasia kuzihimiza Urusi na China kuunga mkono juhudi hizo.

Bi Merkel amesema anaamini Saudi Arabia itaunga mkono juhudi za Ujerumani kutaka kuongeza sheria za kudhibiti masoko ya fedha kwenye mkutano wa nchi 20 tajiri duniani utakaofanyika nchini Canada mwezi ujao. Hata hivyo amesema ana wasiwasi ikiwa Saudi Arabia itaunga mkono wazo la Ujerumani kutaka kodi itozwe kwa biashara ya fedha ya kimataifa, kwa kuwa uchumi wa nchi hiyo uko imara kutoka na mauzo ya mali asili.

Kansela Merkel amemshukuru mfalme Abdula kwa hatua ya maafisa wa usalama wa Saudi Arabia kuwaokoa wasichana wawili wa Kijerumani, ambao walikuwa wakizuiliwa mateka nchini Yemen kwa takriban mwaka mmoja.

Bi Merkel pamoja na ujumbe wa wafanyabiashara wa Ujerumani aliwasili jana jioni Saudi Arabia akitokea Abu Dhabi, na kuandaliwa dhifa ya kitaifa na mwenyeji wake mfamle Abdullah katika mji wa bandari wa Jeddah.

VAE Golf-Staaten Angela Merkel in Abu Dhabi
Kansela Angela Merkel, kushoto, na rais wa jumuiya ya falme za kiarabu Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan huko Abu DhabiPicha: AP

Akiwa Abu Dhabi, kansela Merkel alikutana na rais wa famle za Kiarabu Sheikh Khalifa bin Zayed al Nahyan na kusema kuna haja kwa Ujerumani kuimarisha ushrikiano wake na nchi za ghuba.

"Nadhani hili ni mojawapo a maeneo muhimu yenye maendeleo ya kiuchumi. Tunakabiliwa na ushindani mkubwa katika ushirikiano wa kiuchumi kutoka kwa nchi za Asia kwa mfano Korea Kusini na China. Ujerumani inaweza kuhimili mashindano haya, lakini hiyo ina maana tunanatikwa kuimarisha uhusiano wetu na eneo hili. Na nadhani huo ni uwekezaji mzuri."

Hapo jana, Bi Merkel alikitembelea chuo kipya cha sayansi na teknolojia cha Mfalme Abdullah, mojawapo ya miradi muhimu katika mpango wa mfamle Abdullah kuijenga Saudi Arabia kuwa taifa la kisasa.

Chuo hicho cha kimataifa cha kufanyia utafiti kilicho kilomita 80 kaskazini mwa Jeddah kimezungukwa na kuta ndefu na huwaruhusu wanafunzi wa kike na wa kiume kuchangamana pamoja kinyume na maeneo mengine ya Saudi Arabia ambako sheria za kiislamu haziwaruhusu wanawake na wanaume kuchangamana. Katika chuo hicho, kansela Merkel amejionea mahabara zenye vifaa na mashine zilizonunuliwa kutoka Ujerumani.

Hii leo kansela Merkel na ujumbe wake wa wafanyabiashara wa Ujerumani anatarajiwa kufanya mikutano kadhaa mjini Jeddah kabla kwenda Qatar na Bahrain.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/DPAE

Mhariri: Aboubakary Liongo