1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel kuizuru China

P.Martin24 Agosti 2007

Siku ya Jumapili,Angela Merkel atafanya ziara yake ya pili nchini China kama Kansela wa Ujerumani.Je,Wachina wanamuonaje Kansela wa Ujerumani?

https://p.dw.com/p/CH97
Kansela wa Ujerumani,Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani,Angela MerkelPicha: AP

Kansela wa Ujerumani anajulikana miongoni mwa raia wa Kichina,hata ikiwa hapo mwanzoni alitazamwa vingine kulinganishwa na mtangulizi wake Gerhard Schroeder.

Kwa maoni ya Profesa Gu Junli alie mtafiti mashuhuri kuhusu masuala ya Ujerumani katika Taasisi ya Elimu ya Jamii,uhusiano wa Ujerumani na China ulibadilika kidogo baada ya serikali ya mseto kushika madaraka chini ya uongozi wa Kansela Merkel.Profesa Gu anasema,sababu mojawapo ni msimamo mpya wa siasa za nje za Ujerumani kuikaribia zaidi Marekani.Pili ni kwamba Merkel na wanasiasa wenzake bado hawaifahamu China vizuri.Sababu ya tatu aliyotoa inashangaza. Amesema hivi:

“Yeye anatokea iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani DDR.Na aliishuhudia serikali ya wakati huo ya SED.Na huiona China inayoongozwa na chama cha Kikomunisti ikifanana kidogo na iliyokuwa DDR.“

Labda ni yale maisha aliyoshuhudia chini ya uongozi wa kidikteta katika enzi ya DDR,ilimfanya Merkel kuwasiliana na wanaharakati wa upinzani wakati wa ziara yake ya kwanza nchini China.

Hilo ni jambo ambalo wapinzani wasomi kama Liu Xiaobo hawakusahau.Kwa maoni yake,serikali ya China haishughulishwi na maoni ya ndani ya nchi bali,huhofia ukosoaji kutoka nje.Mbali na kutaka kuonyesha kuwa ni nchi iliyo wazi,China vile vile inataka kufanya biashara na nchi za nje.

Baada ya kuwepo kipindi kifupi cha uhusiano baridi kati ya China na Ujerumani,China imenyosha mkono wa urafiki.Kwa maoni ya Profesa Gu Junli, uhusiano huo ulianza kubadilika,baada ya Rais wa Ujerumani,Horst Köhler kuizuru China katika mwezi wa Mei.

Safari hii,kinyume kabisa na kawaida,ziara ya Merkel imetangazwa magazetini kwenye ukurasa wa mbele.Vile vile kuanzia tarehe 29 Agosti, Ujerumani inawakilishwa kwenye Maonyesho ya Vitabu mjini Beijing.Uhusiano wa miaka 35 kati ya Ujerumani na China utasherehekewa kwa kufunguliwa programu ya kitamaduni ya kila miaka mitatu na Ujerumani pia inaweza kuwakilishwa.

Kinyume na kawaida,kiongozi wa serikali ya China atakuwa na muda mrefu pamoja na Kansela Merkel wakati wa ziara yake nchini China.Wakati huo labda Merkel atafanikiwa kuisadikisha China kuhusu mada yake kuu inayohusika na ulinzi wa mazingira.