1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel ziarani Afghanistan

12 Machi 2012

Merkel yuko Afghanistan kwa ziara ya ghafla kuwatembelea wanajeshi wa Ujerumani wakati hali ya usalama ikiwa imezorota.

https://p.dw.com/p/14JCg
Kansela Angela Merkel akiwa Masar-i-Scharif
Kansela Angela Merkel akiwa Masar-i-ScharifPicha: picture-alliance/dpa

Ziara ya Kansela huyo wa Ujerumani imekuja siku moja baada ya kutokea shambulizi baya kabisa la ufyatuaji risasi lililofanywa na mwanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan,shambulio ambalo sasa limezusha hofu kuanzia Marekani hadi ulaya.

Maafisa wa Marekani wameonya juu ya uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kulipiza kisasi baada ya mwanajeshi wa nchi hiyo kuua raia wasiokuwa na hatia. Tangazo la Ubalozi wa Marekani mjini Kabul limewatahadharisha wamarekani kuwa kuna hatari ya kupanda kwa hisia dhidi ya Marekani kwa siku na wiki zijazo hususan katika majimbo ya kusini.

Baada ya mwanajeshi wa Marekani kuvamia nyumba za raia na kuua watu kumi na sita, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, serikali ya Marekani imechukua hatua za haraka kutenganisha uhalifu wa mwanajeshi huyo na mienendo ya jumla ya wnajeshi wengine wa nchi hiyo wapatao 90,000 nchini Afghanistan. Hata hivyo inasadikika kuwa mauaji hayo yaliyofanywa kwenye jimbo la kusini la Kandahar jana yatachochea hasira dhidi ya nchi za magharibi.

Ni tukio ambalo limekuja takribani wiki tatu baada ya wanajeshi wa Marekani kuchoma kitabu kitakatifu cha waislamu, Koran, katika hali ambayo ilielezwa kuwa ni 'kukosekana kwa uangalifu'. Kitendo hicho kilifuatiwa na ghasia ambamo watu 30 waliuawa.

Rais wa Marekani Barack Obama amesema amesikitishwa mno na mauaji ya jana, na amempigia simu rais wa Afghanistan Hamid Karzai kuahidi kuwa uchunguzi utafanyika haraka kujua ukweli juu ya kisa hicho, na yeyote anayehusika atawajibishwa ipasavyo.

''Kisa hiki ni cha kutisha na kusikitisha, na hakiwakilishi nidhamu murua ya jeshi letu na heshima ambayo Marekani inayo kwa wananchi wa Afghanistan.'' Alisema Obama katika ujumbe wake.

Ujumbe kama huo wa Rais Obama umetolewa pia na balozi wa Marekani nchini Afghanistan, James Cunningham aliyesema kwamba,wanachukizwa na shambulio lolote linalofanywa na mwanajeshi wa Marekani dhidi ya raia, na kulaani ukatili wowote dhidi ya raia. Amewaahidi wananchi wa Afghanstan kwamba mtu, au watu waliohusika katika katika kisa hiki cha kutisha, watatambuliwa na kufikishwa mbele ya sheria.

Visa kama hiki huchochea chuki za waafghanistan dhidi ya nchi za magharibi, na hutumiwa na wanamgambo kwa faida yao. Tayari kikundi cha Taliban kimesema kitalipiza kisasi.

Wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan
Wanajeshi wa Marekani nchini AfghanistanPicha: picture-alliance/Photoshot

Uhusiano kati ya Rais Hamad Karzai wa Afghanistan na nchi za magharibi zinazomuunga mkono, ambao ni wa mashaka nyakati za kawaida, umekuwa mgumu zaidi. Mauaji ya raia wa Afghanistan ni suala ambalo limeleta msuguano katika uhusiano kati ya Marekanai na Afghanistan.

Kuna taarifa zinazopingana juu ya idadi ya watu waliofanya mauaji haya dhidi ya raia. Wananchi walioshuhudia yakitokea wanasema wanajeshi wengi walihusika, lakini jeshi la Marekani limesema ni mwanajeshi mmoja tu aliyehusika.

Mauaji ya jana yanaweza pia kuimarisha hisia zinazozidi kukua mjini Washington, juu ya mafanikio ya vita vya Afghanistan hata baada ya kuongeza idadi ya wanajeshi, ambako kulikuwa na makusudi ya kushinda vita hivi.

Vita hivi tayari vimekwishaigharimu Marekani dola bilioni 500, na wanajeshi wake 1900 wamekwishauawa. Jumla ya wanajeshi wote wa kigeni waliokufa nchini Afghanistan inazidi 3000.

Mwandishi: Daniel Gakuba/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu