1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel ziarani Dubai na Kuweit

Oummilkheir6 Februari 2007

Kansela Angela Merkel akamilisha ziara yake ya Mashariki ya kati hii leo

https://p.dw.com/p/CHKi
Kansela Merkel ahutubia mkutano wa wanauchumi mjini Abu Dhabi
Kansela Merkel ahutubia mkutano wa wanauchumi mjini Abu DhabiPicha: AP

Kansela Angela Merkel anaendelea na ziara yake ya Mashariki ya kati kwa kuitembelea Dubai hii leo.Baadae leo mchana anatazamiwa kwenda Kuweit.Lengo la ziara ya kansela Angela Merkel katika eneo hilo ni kujaribu kufufua juhudi za amani ya mashariki ya kati ,hali nchini Irak na mzozo uliosababishwa na mradi wa kinuklea wa Iran.

Baada ya Misri,na Saud Arabia,jana kansela Angela Merkel alizitembelea falme za nchi za kiarabu.Mara baada ya kuwasili Abudhabi,kansela Merkel alikutana na kiongozi wa Emirat Cheikh Khalifa Ben Zayed Al Nahayan na kuzungumzia mzozo wa Palastina,hali nchini Irak na Libnan pamoja na mzozo uliosababishwa na mradi wa kinuklea wa Iran.

Kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran kansela Angela Merkel alisema:

„Kuna watu katika eneo hili na kwengineko,ambao hawataki kuona juhudi zikifanikiwa.Ndio maana tumeingiwa na hofu na hasa kuhusiana na Iran linapohusika suala la mradi wake wa kinuklea.“

Sheikh Khalifa Ben Zayed Al Nahayan amesifu juhudi za Ujerumani kuelekea Mashariki ya kati na hasa katika kufufua utaratibu wa amani kati ya Israel na Palastina.

Kansela Angela Merkel amezungumzia uungaji mkono wa Umoja wa ulaya kwa mazungumzo yanayofanyika leo hii Makka kati ya ndugu wanaohasimiana wa Palastina.Amehakikisha pia Ujerumani itafanya kila liwezekanalo ili mazungumzo hayo yafanikiwe.

Akizungumza jana usiku mbele ya wanauchumi wa Emirat katika mkutano kuhusu changamoto zinazoikabili siasa ya nje ya Umoja wa ulaya,kansela Angela Merkel amesisitiza ufumbuzi wa mzozo kati ya Israel na Palastina ni muhimu ili matatizo mengine ya eneo hilo yaweze kufumbuliwa.

Kanselas Angela Merkel ameshadidia:

„Suala hapa ni kwamba jumuia nzima ya kimataifa inatoa ishara ya pamoja inayomaanisha:Tuna amini fikra ya ufumbuzi wa madola mawili-Israel na Palastina na uwezekano wa kuishi pamoja kwa amani.Na nionavyo mie,imani hiyo tunabidi tufanye kila liwezekanalo kuitekeleza.“

Kansela Angela Merkel ameondoka Abu Dhabi leo asubuhi kuelekea Dubai ambako amepangiwa kukutana na makamo wa rais na waziri mkuu wa-Emirat ambae pia ni mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed ben Rashid Al Maktoum .

Kansela Angela Merkel alitokea Riyadh ambako alikutana pia na katibu mkuu wa baraza la ushirikiano la Ghuba-Abderrahmane Al Attiyah,na kuzungumzia makubaliano ya biashara huru kati ya Umoja wa ulaya na baraza hilo la Ghuba linalozileta pamoja Saud Arabia ,Bahrein,Emirat,Kuweit,Oman na Qatar.

Kansela Angela Merkel anatazamiwa kuondoka Dubai leo mchana na kuelekea Kuweit,kabla ya kurejea nyumbani nchini Ujerumani leo usiku.