1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Scholz ahimiza mshikamano katika Umoja wa Ulaya

Saumu Mwasimba
29 Agosti 2022

Hotuba ya Kansela Scholz mjini Prague yatilia mkazo mageuzi katika Umoja wa Ulaya yanayolenga kuongeza wanachama zaidi

https://p.dw.com/p/4GBLo
Tschechien | Olaf Scholz in Prag
Picha: Petr David Josek/AP Photo/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz leo ametoa ahadi ya kuiunga mkono kwa dhati Ukraine na nchi nyingine zenye matumaini ya kujiunga na Umoja wa Ulaya,ingawa wakati huohuo amesisitiza kwamba kuiongeza jumuiya hiyo kuwa na wanachama 30 au 36 kutahitaji yafanyike mageuzi.

Kansela wa Ujerumani  Olaf Scholz ameweka wazi kwamba yuko tayari kuziunga mkono nchi sita za magharibi katika eneo la  Balkan,Moldova,Georgia na Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya ingawa pia amebaini wakati jumuiya ikitanuka kura ya turufu ambayo ni haki ya kila nchi mwanachama itakazimika kuondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na mfumo wa kura ya wengi.

Tschechien | Olaf Scholz in Prag
Picha: Petr David Josek/AP Photo/picture alliance

Mageuzi hayo hasa yana dhamira ya kutocheleweshwa hatua ya kuchukuliwa maamuzi na Umoja huo. Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni suala ambalo lilishawahi kuutia kwenye majaribu mfumo wa maamuzi ya pamoja katika wakati ambapo ilihitajika kuchukuliwa maamuzi ya hatua ya pamoja.

Kansela huyo wa Ujerumani akizungumza katika chuo kikuu cha Charles mjini Prague, ameitaka jumuiya hiyo kutafuta misimamo ya pamoja akitowa mfano wa kutumika njia ya upigaji kura katika masuala ambayo hasa hasa yanahitaji wazungumze kwa sauti moja,kama suala la sera ya vikwazo au masuala yanayohusiana na haki za binadamu. Scholz  amezitolea mwito nchi za Umoja wa Ulaya kukubaliana na mageuzi ambayo yataisaidia jumuiya hiyo kukabiliana na migawanyiko na kusimama  pamoja dhidi ya maadui wa nje kama vile Urusi na China.

"Athari za hili kwa Ulaya huenda ikabainishwa kwa mukhtasari kama ifuatavyo-Tunapaswa kushirikiana,kuitatua migogoro ya zamani  na kutafuta hatua mpya za suluhu. Hilo huenda likaonekana suala la kawaida tu lakinini kuna mengi ya kufanywa nyuma ya kauli hii.''

Karls-Universität in Prag
Picha: Peter Erik Forsberg/IMAGO

Lakini pia ameweka wazi kwamba Ujerumani itaimarisha kwa kiwango kikubwa mifumo yake ya ulinzi wa anga na kuitengeneza katika njia ambayo kwamba inaweza pia kuzilinda nchi nyingine jirani za Ulaya kuanzia zile za eneo la Baltic hadi Skandinavia.

Hakutowa maelezo ya kina kuhusu mfumo huo japo mnamo mwezi March aligusia mipango ya kununua kutoka Israel mifumo ya kuzuia makombora ambayo inaweza pia kuzikinga nchi jirani la Umoja wa Ulaya.Hotuba yake ya Prague imegusia vitu vingi lakini ikisisitiza zaidi juu ya ulazima ya Umoja wa Ulaya kujiweka tayari kwa ajili ya mustakabali wake wa baadae wa kuwa na wanachama zaidi ya 27.

Kadhalika ameunga mkono miito ya kutaka muundo wa bunge la Ulaya ambalo kwa sasa lina wabunge 751 utathminiwe tena ili kuepusha  bunge hilo kufurika pale jumuiya ya Umoja wa Ulaya itakapotanuka. Hata hivyo mapendekezo yaliyotolewa huenda yasipokelewe na nchi ndogo ambazo zinakhofia mageuzi katika Umoja huo wa Ulaya yanaweza kuuteka nyara mfumo mzima wa  kutowa maamuzi.