1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani, Bibi Merkel, anamaliza ziara Uchina

28 Agosti 2007

Katika ziara yake ya Uchina, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekutana na watu wazito katika siasa za Uchina, nao ni rais wa chama tawala na mkuu wa nchi, Hu Jintao, na waziri mkuu Wen Jiabao. Matokeo hasa hayajulikani, licha ya kuweko hali jumla ya kuboreka uhusiano baina ya nchi zao mbili.

https://p.dw.com/p/CH8y
Kansela wa Ujerumani, Bibi Angela Merkel, na Rais wa Uchina, Hu Jintao, wakitakiana heri na furaha.
Kansela wa Ujerumani, Bibi Angela Merkel, na Rais wa Uchina, Hu Jintao, wakitakiana heri na furaha.Picha: AP

Uhusiano baina ya Ujerumani na Uchina sio ulio rahisi, lakini ni muhimu. Kwa hivyo, licha ya matatizo yote, mtu inafaa abakie akizungumza na Uchina.

Kwa wanasiasa wa Ujerumani, kufanya ziara rasmi katika Uchina ni shughuli ilio ngumu, na hiyo inatokana na matarajio tafauti yanayowekewa na kila upande katika ziara kama hizo. Hali hiyo imeongezeka kutokana na malalamiko dhidi ya Uchina ambayo yanaonekana hadharani- habari kutoka nchi hiyo kuhusu kuendelea kukanyagwa haki za binadamu, kutengenezwa bidhaa za sumu viwandani na uhalifu unaofanywa juu ya mazingira. Lakini kati ya hao wanaofanya ziara huko Uchina wako wawakilishi wa viwanda ambao wanataka kupata msaada wa wanasaiasa ili wajipatie kandarasi kubwa kubwa, lakini wakati huo huo wanapinga mtindo wa Uchina wa kuiba haki miliki za watu wa nchi za nje.

Uchina katika mazungumzo inashiriki kwa kujiamini sana, na hiyo inatokana na neema kubwa ya kiuchum ambayo nchi hiyo inajionea kwa miongo miwili sasa, na pia kutokana na mabadiliko ya wizani wa nguvu duniani.

Lakini Uchina, wakati huo huo, inatambua juu ya sura mbaya inayoipata. Ndio maana wakuu wa Uchina wanajaribu kuiboresha sura hiyo, walimkubalia Bibi Merkel yale aliyoyataka katika mazungumzo, lakini hawasemi hasa nini wanachoahidi kufanya. Hivyo ndio maana mengi yalioonekana katika ziara ya BibI Merkel ni alama; kutoka bendera za Ujerumani kupepea katika Uwanja wa Tiananmen, kuonekana picha za Bibi Merkel katika magazeti ya Uchina hadi ishara za kibinafasi, kama vile Bibi Merkel kutembea pamoja kwa miguu na waziri mkuu Wen Jiabao. Hii ni kuendeleza mtindo ulioanza mwaka mmoja sasa ya kuweko diplomasia ya kufanya mazungumzo huku viongozi wakitembea pamoja kwa miguu.

Katika upande huu, Kansela Angela Merkel kweli ameusogeza mbele msimamo wake, na amezielezea mada zinazomgusa. Tena bila ya vishindo. Amefanya hivyo kwa sauti ya upole, kwa mtindo wa urafiki ambao mtangulizi wake, Kansela Gerhard Schroader ilibidi aupate kutoka kwa viongozi wenzake wa kiume. Bibi Merkel hajaliacha pembeni suala lolote ambalo ni zito, kama ni kuheshimiwa haki za binadamu, kulindwa haki miliki za wavumbuzi au ulinzi wa mazingira. Na mwishoni aliumaliza usanii wake kwa kutojifanya kuwa ni mwalimu wa kuwasomesha Wachina nini yafaa wafanye.

Mtu akipenda asipende, matatizo mengi yalio muhimu duniani hayawezi kutanzuliwa bila ya Uchina. Moja ya matatizo hayo ni mabadiliko ya hali ya hewa duniani, bila ya kusahau pia mzozo wa Korea Kaskazini kuwa na na silaha za kinyukliya, mpango wa kinyukliya wa Iran na mzozo wa Darfur katika Sudan. Hakuna mbadala: lazima mtu abakie anazungumza na Uchina, na ni uzuri kwamba Kansela Angela Merkel anafanya hivyo. Lakini Uchina, kwa upande wake, itambuwe kwamba inachukuliwa kutokana na kauli zake.

Kwa mfano, waziri mkuuwa Uchina, Wen Jiabao, kwa kauli yake mwenyewe, amesema kwamba wao hawatafanya makosa ya kwanza kuyachafua mazingira na baadae kuyatengeneza upya mazingira hayo. Hayo ni maneno mazuri! Sio maisha tu kuutolea mhanga msingi wa maisha ya mamilioni ya watu kwa ajili tu ya kupata faida za haraka za fedha. Na ikiwa waziri mkuu huyo hawezi kuyatunza mazingira, basi yafaa amlinde mtu yeyote ambaye anapigania ulinzi wa mazingira hayo- kama vile mwanaharakati Wu Lihong. Bwana huyo kwa zaidi ya miaka kumi sasa anapigania kunusuriwa bwawa la Taihu, la tatu kwa ukubwa katika Uchina. Badala ya kutunukiwa nishani, bwana huyo katikati ya mwezi huu wa Agosti alipewa kifungo cha miaka mitatu gerezani . Makosa yake: aliifanyia tafrani duru ya makada wa kibepari huko Uchina.