1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani ziarani China

P.Martin27 Agosti 2007

Mada kuu za Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakati wa ziara yake nchini China ni uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili na njia za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani

https://p.dw.com/p/CH95
Kansela Angela Merkel(kulia) akikagua gwaride la heshima alipopokewa na Waziri Mkuu Wen Jiabao(kushoto) mjini Beijing
Kansela Angela Merkel(kulia) akikagua gwaride la heshima alipopokewa na Waziri Mkuu Wen Jiabao(kushoto) mjini BeijingPicha: AP

Kansela Angela Merkel anaefuatana na ujumbe mkubwa wa wafanya biashara katika ziara yake ya siku tatu nchini China,amekaribishwa na waziri Mkuu Wen Jiabao kwa heshima kubwa.

Wen Jiabao amesema,uhusiano kati ya China na Ujerumani ni mzuri mno na akasisitiza kuwa chini ya uongozi wa Merkel,uhusiano huo haukudhoofika bali umeimarika.

Baadae mbele ya viongozi hao wawili,wajumbe wa kampuni ya Kijerumani ya Thyssen-Krupp na China walitia saini mkataba wenye thamani ya kama Euro milioni 150.Mkataba mwingine uliotiwa saini unahusika na mada iliyoshughulikiwa sana na Merkel-nayo ni njia za kuhifadhi mazingira duniani.

Kwa mujibu wa ripoti za kimataifa,China imeipita Marekani na sasa ni mchafuzi mkubwa kabisa wa mazingira duniani.China imeathirika vibaya kwa uchafuzi wa mazingira,ikisemekana kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mito yake imechafuliwa.

Hata hivyo,Waziri Mkuu Wen Jiabao amesisitiza, nchi yake ipo tayari kushghulikia zaidi hatua za kuhifadhi mazingira na hali ya hewa duniani.

Mbali na suala la mazingira,Kansela Merkel pia anataka kuzungumzia haki za binadamu.Kabla ya kuanza ziara yake nchini China,Merkel alisisitiza hivi:

“Uhusiano wetu wa kiuchumi ni mzuri,na hata uhusiano wa kisiasa ni wa karibu sana;kwa hivyo ni dhahiri kuwa tutajadili waziwazi hata masuala ambayo labda ni ya utata kama vile haki za binadamu na ubora wa bidhaa.“

Ni dhahiri kuwa suala la haki za binadamu haliwezi kuepukwa.Kwa mujibu wa kundi la „Waandishi wa habari wasio na mipaka“,mkosoaji wa serikali ya Beijing,Lu Gengsong,alikamatwa siku ya Ijumaa.Muandishi huyo katika mtandao wa Internet alieleza kuhusu hali ya haki za binadamu inayokutikana nchini China.Kwa mujibu wa kundi hilo,nchini China hivi sasa,si chini ya waandishi wa habari 30 na watumizi 50 wa mtandao wa Internet wametiwa ndani.

Wakati huo huo,suala la kuheshimu hati miliki na vile vile kuhusu ubora wa bidhaa ni masuala yaliyokuwepo katika ajenda ya Kansela Merkel kabla ya kuelekea Japan siku ya Jumatano.