1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani ziarani nchini China

P.Martin27 Agosti 2007

Kansela Angela Merkel akifanya ziara yake ya pili nchini China tangu kushika uongozi wa serikali ya Ujerumani,ametoa mwito kwa China kufanya bidii zaidi,kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa duniani na vile vile kuhifadhi haki miliki.

https://p.dw.com/p/CH93
Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu Wen Jiabao walipowasili Ukumbi Mkuu mjini Beijing
Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu Wen Jiabao walipowasili Ukumbi Mkuu mjini BeijingPicha: AP

Kabla ya kuanza ziara yake nchini China,Merkel alisema,atazungumza waziwazi masuala ya ubishi pia.Hii leo akiendelea na mkakati wake wa kuwa na mazungumzo waziwazi alisema,kila nchi ina haki ya kuwa na maendeleo,lakini katika biashara ya kimataifa ni lazima kufuata kanuni za kimsingi.

Akaongezea kuwa kanuni za kukusanya malighafi zinapaswa kuwa sawasawa,kwa kila taifa duniani,ikidhihirika kuwa hapo,ameashiria uhusiano wa China na Sudan.Kwani China ina maslahi makubwa nchini Sudan na inashinikizwa na jumuiya ya kimataifa kuutazama upya uhusiano wake na Khartoum,baada ya kutuhumiwa kuwa misaada ya Beijing inazidisha machafuko katika jimbo la magharibi la Sudan,Darfur.

Wakati wa majadiliano yake pamoja na Waziri Mkuu Wen na Rais Hu Jintao mjini Beijing,Merkel alisema,China ambayo mwakani itakuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiks,inatazamwa na ulimwengu mzima hivi sasa.Akamuambia Rais Hu,Ujerumani na China zinapaswa kufanya kazi pamoja katika masuala ya haki za binadamu,ulinzi wa haki miliki na mazingira na vile vile kwenye sekta ya biashara.

Kwa upande mwingine,Waziri Mkuu Wen Jiabao alipozungumzia suala la ulinzi wa mazingira alisema,kulinganishwa na Ujerumani,ni vigumu zaidi kwa China kupunguza gesi inayochafua mazingira.Sababu ni kuwa China ina watu wengi zaidi na haijafikia ukuaji wa kiuchumi wa nchi zilizoendelea kiviwanda katika pato la ndani la kila mwananchi mmoja.Akaongezea kuwa,kwa sehemu fulani,China imechangia uchafuzi wa mazingira katika kipindi cha miaka 30 tu,wakati nchi za viwanda zikiendelea kufanya hivyo tangu miaka 200 iliyopita.

Mnamo mwezi wa Juni katika mkutano wa kilele ulioongozwa na Merkel nchini Ujerumani,viongozi wa nchi zilizoendelea kiwanda G-8 walikubali kupunguza gesi zinazochafua mazingira na kufanya kazi pamoja na Umoja wa Mataifa,kupata makubaliano mapya kuhusu njia za kupambana na ongezeko la joto duniani.

Kansela Merkel kesho Jumanne,amepanga kukutana na waandishi mbali mbali kuzungumza juu ya uhuru wa uandishi wa habari nchini China.