1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Wa Ujerumani ziarani nchini Israel

17 Machi 2008

Siku ya Jumapili Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alianza ziara yake ya siku tatu nchini Israel.Alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Tel Aviv alipokewa na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert.

https://p.dw.com/p/DPVM
German Chancellor Angela Merkel, left, and Israel's Prime Minister Ehud Olmert, right, at the official welcoming ceremony for Merkel at Ben Gurion airport in Tel Aviv, Sunday March 16, 2008. Merkel will spend three days touring the Jewish nation and strengthening ties between Berlin and Jerusalem. (AP Photo/Ariel Schalit)
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel(kushoto)akipokewa na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert kwenye uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv.Picha: AP

Angela Merkel na Ehud Olmert wakasisitiza dhamira ya kuwa na urafiki wa kudumu kati ya nchi hizo mbili.Baada tu ya Kansela wa Ujerumani kupokewa kwa heshima ya kijeshi kwenye uwanja wa ndege wa Ben Gurion,viongozi hao wawili kwa ufupi walieleza wazi wazi lengo la ziara rasmi ya Merkel huku Israel ikiadhimisha miaka 60 tangu kuundwa kwa taifa hilo.Moja ni kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kuwa na maelewano ya karibu katika takriban masual yote ya kisiasa na kiuchumi.

Kansela Merkel kwa upande wake amesema,yeye anataka kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wa Israel na Ujerumani.Na Ehud Olmert akimsifu Kansela wa Ujerumani alisema,Merkel ni mshirika muhimu wa Israel barani Ulaya na katika jumuiya ya kimataifa ambae huzingatia maslahi ya usalama wa Israel.Waziri Mkuu wa Israel akaitumia fursa hiyo kugusia suala la nyuklia la Iran kama alivyofanya alipomkaribisha Rais wa Marekani George W.Bush miezi miwili iliyopita.

Takriban wanasiasa wote wa Israel wanafahamu kuwa baada ya Marekani,Ujerumani ndio mshirika muhimu kabisa wa Israel.Kwa hivyo katika siasa za kigeni,Olmert anatazamia kuwa Merkel atazidi kuunga mkono jitahada za jumuiya ya kimataifa kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia kwa kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi.

Kansela wa Ujerumani aliposhika madaraka miaka miwili na nusu iliyopita alipitisha maamuzi ya maadili yaliyothaminiwa sana nchini Israel na kuongeza hadhi yake na bila shaka Ujerumani pia imenufaika.Merkel bila ya kusita huitetea Israel na siasa za serikali hiyo.Hapo,Merkel kama watangulizi wake anafuata sera ya kigeni ya Ujerumani isiyobadilika,kuhakikisha usalama wa Israel kwa sababu ya kuwajibika kutokana na historia yake inayohusika na mauaji ya Wayahudi milioni sita wakati wa utawala wa Manazi.

Je,Kansela alipokuwa akizungumzia mradi wa nyuklia wa Iran alimaanisha nini aliposema"vitisho vyo vyote dhidi ya Israel ni vitisho dhidi yetu pia?"

Merkel wakati wa ziara yake nchini Israel,huenda akafanikiwa kuupa uhusiano wa Ujerumani na Israel msukumo mpya au hata mwelekeo mpya.