1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KARBALA:Muda wa kutotembea watangazwa na Waziri mkuu

29 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBUm

Waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki ametangaza muda wa kutotembea mjini Karbala baada ya mapigano makali kutokea na kusababisha vifo vya watu 52.Maelfu ya Washia wanakutana mjini humo ili kuadhimisha sherehe ya kidini ya Kishia ya Shabaniya.

Bwana Maliki anawalaumu wafuasi wa kiongozi wa zamani wa Iraq marehemu Saddam Hussein kwa kuanzisha ghasia hizo.Majeshi ya usalama ya Iraq yanadhibiti mji kwa sasa.Muda huo wa kutotembea ulianza saa moja za London na unahusisha watu pamoja na magari kwa mujibu wa tangazo la televisheni ya kitaifa.

Kulingana na mwandishi wa habari wa AFP mjini Karbala mapigano kati ya wapiganaji wa kishia na polisi yalianza jana na kuendelea usiku kucha.Wapiganaji hao wa Kishia walikusanyika karibu na mji wa kale ulio na madhabahu mawili ya Imam Hussein na Imam Abbas yaliyo tukufu zaidi na lengo la hijja yenyewe.

Waziri Mkuu Nuri al Maliki anayeshinikizwa nchini mwake na jamii ya kimataifa kwa kutodumisha amani Iraq analaumu makundi ya uhalifu yaliyosalia baada ya utawala wa marehemu Saddam Hussein kumalizika.

Mapigano hayo yalisababisha mahujaji hao kutoroka.Sherehe za Shabaniya ni za kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Imam Mohammed al Mahdi katika karne ya 9.Imam huyo wa 12 wa kishia alipotea mjini Samarra na kuepuka mauti ila atarejea kuuokoa ulimwengu.