1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Karlsruhe yatarajiwa kuamua

Hamidou, Oumilkher11 Septemba 2008

Jee fedha za usafiri toka mahala mtu anakoishi na kule anakofanya kazi ziendelee kulipwa au vipi?

https://p.dw.com/p/FG3k
Wafanyakazi wameingia njiani kwenda kaziniPicha: AP




Wahariri wengi hii leo wanakodowa macho yao mjini Karlsruhe,ambako korti kuu ya katiba inatazamiwa kupitisha uamuzi kuhusu malipo ya fedha zinazofidia masafa kati mahala mtu anakoishi na kule anakofanya kazi.Zaidi ya hayo,wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamezungumzia zoezi la kisayansi mjini Geneva kuigiza mpasuko wa "Big Bang" na kuibuka ulimwengu wetu.


Tuanze lakini na mada ya kwanza.Gazeti la OSTSEE-ZEITUNG la mjini Rostock linahoji:


"Kutokana na sababu mbali mbali,utakuta kwamba wafanyakazi wengi hawana njia nyengine isipokua ,kuingia magarini,ndani ya treni au mabasi,siku nenda siku rudi, ili kuweza kufika makazini mwao-bila ya kujali wanasafiri masafa ya kilomita mia moja au kumi tuu.Ni adha isiyo ndogo hiyo na anaeiangalia hali hiyo kua ni starahe, basi hana imani."



Gazeti la RHEIN-NECKAR-ZEITUNG la mjini Heidelberg lina maoni tofauti na hayo,na linaandika:



"Kuna wanaoyakosoa malipo ya wanaofanya kazi mbali na mahala wanakoishi na kufika hadi ya kuyaita "malipo ya kuhamia kwengineko.Yanawafanya waajiri nyumba rahisi nje ya miji,ambako mazingira hayajachafuliwa,ili waweze kufanya kazi mijini na kulipwa mishahara mikubwa mikubwa.Mpango huo una ila chungu nzima ikiwa ni pamoja na kutumiwa ardhi ili kujenga majumba mepya na njia kuu,msongamano wa magari na kuchafuliwa mazingira."


Nalo gazeti la MITTELBAYERISCHE ZEITUNG linanadika:


"Hakuna anaeweza kuashiria kama kila mwenye kumiliki nyumba katika maeneo ya nje ya miji,ataendelea kufaidika na kupatiwa ruzuku ya serikali milele.Tutaraji kwamba mwenyekiti wa chama cha CSU Erwin Huber na  wanasiasa wengine wanaojipendekeza kama yeye,hoja zao zitashindwa mbele ya mahakama ya katiba mjini Karlsruhe."


Mahkama hiyo ya katiba ina muda wa hadi mwisho wa mwaka huu kuamua kama utaratibu ulioanzishwa tangu mwaka 2007 uendelee kutumika au la.Gazeti la Frankfurter Rundschau linahisi:


"Nafasi iliyoko ni ya nusu bin nusu.Baadhi ya majaji wanaonyesha kuvutiwa na msimamo wa waziri wa fedha Steinbruck;unaomaanisha "sio lazma watu walipwe fedha za usafari".Hata hivyo tusubiri tuone wezani wa kisheria utaelemea upande gani.Kimoja hata hivyo ni dhahiri:malipo ya fedha za usafiri yamepitwa na wakati."


Kuhusu mada ya pili magazetini,gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT linajiuliza kama kweli kulikua na haja ya kupoteza yuro bilioni sita eti kwasababu ya kutaka kujua zaidi kuhusu anga za juu,mripuko wa Big Bang na vyenzo vyenginevo vya maumbile?


Si afadhali fedha hizo,uhandisi,na ujuzi ungetumiwa kutibu magonjwa badala ya kutengeneza chombo cha kuharakisha mripuko wa Big Bang?Sahihi ni kwamba bila ya utafiti wa kina hatuwezi kubuni fikra mpya.Bila ya fikra msingi za Albert Einstein tusingekua hii leo na chombo cha gari cha kuongoza safari barabarani,bila ya utafiti wa anga za juu tusingekua na majiko ya kupikia ya kimambo leo.Kwa hivyo pengine enzi ya maana ya utafiti imechipuka kutokana na utafiti huu wa kwanza wa hali ya juu kwa maisha ya binaadam.