1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Karzai aweka kiwingu katika mazungumzo na Bush.

Sekione Kitojo6 Agosti 2007

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai anafanya ziara nchini Marekani leo Jumatatu na anatarajiwa kukamilisha mazungumzo na rais George W. Bush yatakayohusu hali inayozidi kuporomoka ya kiusalama nchini humo baada ya kushangaza wengi nchini Marekani kwa kuitaja Iran nchi inayoangaliwa kuwa ni hasimu mkubwa wa Marekani , kama rafiki mkubwa badala ya adui.

https://p.dw.com/p/CHA0
Karzai (kulia) urafiki wa mashaka na Bush? Karzai ameieleza Iran kuwa rafiki mkubwa wa nchi yake Afghanistan.
Karzai (kulia) urafiki wa mashaka na Bush? Karzai ameieleza Iran kuwa rafiki mkubwa wa nchi yake Afghanistan.Picha: AP

Hamid Karzai mmoja kati ya washirika wakubwa wa rais Bush , pia amefichua juhudi za kumtafuta mpangaji mkuu wa mashambulizi ya kigaidi Osama bin Laben hayajaleta mafanikio yoyote katika miaka kadha.

Biashara ya madawa ya kulevywa , maendeleo ya kiuchumi na hatima ya mateka 21 raia wa Korea ya kusini wanaoshikiliwa na kundi la Taliban , zinasemekana kuwa mada muhimu katika mazungumzo ya viongozi hao.

Lakini Karzai , ambaye aliingia madarakani mwaka 2002 akiungwa mkono na Marekani , aliingiza kiwingu katika mazungumzo hayo hata kabla ya kuanza , baada ya kueleza kuwa Iran ni rafiki, nchi ambayo inaonekana na Marekani kuwa inaleta kitisho kwa amani ya dunia.

Katika mahojiano yaliyotangazwa jana Jumapili , Karzai alionekana kukanusha madai ya Marekani kuwa silaha za Iran zinasaidia kuporomosha hali ya usalama nchini Afghanistan.

Matamshi yake hayo yanakwenda kinyume kabisa na msimamo wa Marekani , ambao unaiona Iran kuwa nchi korofi ambayo inatoa msaada wa fedha kwa magaidi, na kuwapa silaha nchini Afghanistan na Iraq na inataka kutengeneza silaha za kinuklia.

Msimamo wa Marekani hata hivyo umesisitizwa tena na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo Condoleezza Rice wakati akitetea uamuzi wa nchi yake wa kuuza silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola kwa Saudi Arabia na mataifa mengine ya ghuba ili kuzuwia nia ya Iran.

Sidhani kama kuna mtu anayetia shaka kuwa Iran ni kikwazo kikubwa, changamoto kwa usalama , kwa marafiki zetu, washirika wetu, na kwa hiyo kwa maslahi yetu pia katika eneo la ghuba, Rice ameiambia televisheni ya CBS.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates , ambaye amerejea hivi karibuni kutoka katika ziara ya mashariki ya kati, amesema akijibu matamshi ya Karzai kuwa , Iran inashiriki katika maeneo yote nchini Afghanistan. Nafikiri, amesema, wasaidia serikali ya Afghanistan lakini wakati huo huo wanasaidia kundi la Taliban, ikiwa ni pamoja na kuwapa silaha.

Ikulu ya Marekani hapo awali imesema kuwa Bush na Karzai watajadili vita vya Marekani dhidi ya ugaidi na kuangalia upya kazi yao ya pamoja ya kuimarisha demokrasia nchini Afghanistan, hali bora na usalama. Karzai pia amedokeza kuwa majeshi ya usalama hayajaweza hata kukaribia kumpata Bin Laden , kuliko hali ilivyokuwa miaka michache iliyopita.

Viongozi hao wawili wanatarajiwa pia kulipa umuhimu suala la mateka wa Korea ya kusini 21, wanaoshikiliwa na Taliban , ambapo wawili kati yao wameuwawa.

Wakati serikali ya Karzai inakataa kutimiza madai ya wateka nyara, serikali ya Korea ya kusini inatoa mbinyo kwa Marekani kuingilia kati.

Mwanadiplomasia mmoja wa Marekani amesema wiki iliyopita kuwa kuna uwezekano wa kutumia mbinyo wa kijeshi dhidi ya Taliban kujaribu kuwaacha huru mateka hao, na kumaliza utekaji huo mkubwa kabisa tangu majeshi ya Marekani kuivamia nchi hiyo miaka sita iliyopita.