1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanajeshi wa Ufaransa ashutumiwa kumnyanyasa mtoto

3 Septemba 2015

Afisa mkuu wa Umoja wa mataifa amesema umoja huo umeanzisha kesi dhidi ya mwanajeshi wa Ufaransa ambaye anatuhumiwa kumdhulumu kingono msichana mdogo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/1GQcI
Mwanajeshe wa Ufaransa wa kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati
Mwanajeshe wa Ufaransa wa kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: AFP/Getty Images/M.Medina

Kumekuwa na madai kadhaa dhidi ya wanajeshi wa Ufaransa kuwadhulumu watoto wadogo wa hata umri wa miaka 9 kwa kuwapa chakula na maji na hatimaye kutaka kufanya ngono nao.Ingawa Ufaransa ilikuwa ikifahamu kuhusu visa vyadhulma ya kingono, visa hivyo vimejitokeza baada ya kuripotiwa na gazeti la Uingereza la Guardian mwezi Aprili.Hakuna aliyekamatwa kufikia sasa.

Balozi wa umoja wa mataifa anayehusika na haki za kibinadamu Zeid Ra´ad Al Hussein ametangaza wakati wa ziara yake katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa mhanga wa dhuluma hiyo alikuwa na umri mdogo wakati wa kisa hicho mwaka mmoja uliopita. Amesema msichana huyo alijifungua mtoto mwezi Aprili na amewasilisha malalamiko yake kwa mamlaka zinazohusika.

Ufaransa yasakamwa na shutuma

Ufaransa ilituma wanajeshi wake kusitisha mapigano katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Desemba mwaka 2013 baada ya vita kuzuka kati ya waislamu na wakristo ambavyo viliwaua watu elfu 5000.

Zeid Raad al-Hussein, Afisa wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki za binadamu
Zeid Raad al-Hussein, Afisa wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki za binadamuPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Tangu wakati huo vikosi vya usalama vimetumwa kuhifadhi amani katika eneo hilo.Walinzi wa amani hao hata hivyo wamekumbwa na shutma za unyanyasaji wa kingono.Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban Ki -moon mwezi uliopita alichukua hatua kwa kumfuta kazi kiongozi wa ujumbe wa umoja huo Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Haya ni madai ya hivi punde ya kutisha ya dhuluma za kingono yanayowakabili wanajeshi wa kigeni katika jamhuri ya Afrika ya kati.Kulingana na al Hussein wanajeshi wa Ufaransa sio sehemu ya ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa. Amesema sharti mbinu itafutwe ya kukabiliana na vitendo vya kinyama vinavyotendwa na wanajeshi popote wanakostahili kulinda raia walio hatarini.

Al-Hussein amesema mamlaka nchini Ufaransa wamefahamishwa na kwamba nchi zinazotoa wanajeshi wanajukumu la kufanya uchunguzi dhidi ya madai hayo haraka iwezekanavyo.

Mwezi uliopita Umoja wa Mataifa uliarifu kuwa madai mengine ya dhuluma za kingono yamewasilishwa kwa Jamhuri ya Afrika ya kati.Madai hayo yanajiri huku Katibu mkuu wa umoja huo Ban Ki Moon akiwa amemfuta kazi kiongozi wa ujumbe wa kulinda amani Babacar Gaye kutokana na ripoti za awali zilizowahusisha wanajeshi wa umoja wa mataifa katika dhuluma za kingono.Chini ya sheria za Umoja wa mataifa mataifa yanayotoa wanajeshi yanalo jukumu la kuwashtaki wanajeshi wanaohusika katika dhuluma zozote.Umoja wa mataifa unasubiri nchi inayohusika katika ripoti za hivi punde kuanza uchunguzi.

Mwandishi:Bernard Maranga/AP/DPA

Mhariri: Gakuba Daniel