1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kashfa ya unyanyasaji wa kijinsia katika kanisa Katoliki yaendelea kutokota.

25 Machi 2010

Maaskofu wawili wanaotuhumiwa na kashfa hiyo wajiuzulu.

https://p.dw.com/p/Mbw6
Baba mtakatifu, Benedict wa 16 aongoza misa, Vatican.Picha: AP

Kulingana na stakabadhi za ushahidi zinazotajwa na gazeti la Marekani la New York Times, Askofu mkuu wa jimbo la Wisconsin alitoa tahadhari kwa kanisa katoliki, idara iliyokuwa ikishughulikia uchunguzi wa visa vya unyanyasaji na iliyoongozwa wakati huo na Baba matakatifu Benedict wa 16, kuhusu mienendo ya kasisi mmoja aliyetuhumiwa kwa kuwanyanyasa kimwili kiasi cha wavulana 200 waliokuwa viziwi lakini hatua yoyote ya kinidhamu haikuchukuliwa dhidi yake.

Stakabadhi hizo zilizowasilishwa na mawakili wanaofuatilia kesi hiyo, zinaonyesha kwamba Askofu Lawrence Murphy aliyefariki mwaka wa 1998, alifanya kazi katika shule ya viziwi ya mtakatifu Yohana kuanzia mwaka wa 1950 hadi 1975 anakotuhumiwa kutekeleza unyanyasaji huo.

Katika taarifa inayoambatana na mustakabali wa kanisa Katoliki, nchini Ireland Askofu John Magee mwenye umri wa miaka 73 wa dayosisi ya Cloyne amejiuzulu baada ya kutuhumiwa kupuuza na kutoshughulikia ipasavyo ripoti za unyanyasaji wa kimwili mwaka jana. Baba mtakatifu Benedict wa XVI amekubali barua yake ya kujiuzulu. Akikiri matukio dhidi yake, Magee aliomba radhi kwa wale aliowakosea. Aliwahi kufanya kazi kama padri msaidizi wa Baba watakatifu watatu wa awali akiwemo, Paul wa XI, John Paul wa I na John Paul wa II.

Maaskofu wengine wanne wanaotuhumiwa na visa hivyo vya unyanyasaji kutoka Ireland wameandika barua za kujiuzulu na kutoka Vatican, Baba mtakatifu amekubali moja tu.

Kwa sasa kuna shinikizo dhidi ya Kadinali Sean Brady wa Ireland kujiuzulu kwa tuhuma za kuhusika kuficha visa vya unyanyasaji wa kimwili wa watoto hasa wakati alipokuwa padri mwaka wa 1975. Kadinali Brady awali alimtetea Askofu Magee aliyejiuzulu na siku ya Jumapili wiki iliyopita akigusia barua ya msamaha ya Baba mtakatifu, alisikika akiwa mkarimu na aliomba uvumilivu kurejesha imani.

Barua ya Baba mtakatifu ya kuomba msamaha kwa waathiriwa wa visa vya unyanyasaji wa watoto Imetajwa na wachunguzi wa maswala ya dini kama iliyokosa mwelekeo wa jinsi ya kukabiliana na washukiwa ikiwemo adhabu na pia haikueleza mikakati ya kubadilisha sera.

Wakati huo huo, Ujerumani imekubali kuanza mazungumzo ya jinsi ya kukabiliana na visa vya unyanyasaji wa kimwili wa watoto vilivyoathiri taasisi na shule kadhaa za kikatoliki nchini humu.

Zaidi ya visa 250 viliripotiwa kwa siku za hivi karibuni na zilizotekelezwa miongo kadhaa iliyopita. Waziri wa masuala ya familia Kristina Schroeder aliwaambia waandishi wa habari kwamba matukio haya ni tatizo katika kanisa.

Mazungumzo hayo ya pamoja yatakayohusisha waathiriwa watakaojitokeza, viongozi husika serikalini na pia mashirika ya kutetea haki za binadam yataanza tarehe 23 mwezi ujao kujaribu kutanzua tatizo hilo sugu na kulizuia katika siku za usoni.

Papst im Gespräch mit Robert Zollitsch tief betroffen über Missbrauchsskandal Flash-Galerie
Baba mtakatifu na Askofu mkuu wa kanisa Katoliki Ujerumani, Zollitsch mwezi huu, Vatican.Picha: picture alliance/dpa

Askofu mkuu Robert Zollitsch wa Ujerumani amelikaribisha wazo hilo na amesema kanisa katoliki litafanya liwezalo ili kuwepo suluhisho la kudumu.

Jarida la 'Stern' limechapisha matokeo ya maoni yaliyokusanywa hapa Ujerumani na linaonyesha kwamba imani ya Wajerumani kwa kanisa Katoliki imepungua kutoka asilimia 29 hadi 19 na umaarufu wa Baba mtakatifu umeshuka kutoka asilimia 38 hadi 24.

Mwandishi: Peter Moss /Reuters/AFP/AP

Mhariri: Josephat Nyiro Charo