1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kashfa zaidi kwa serikali ya Palestina

25 Januari 2011

Al-Jazeera inaarifu kuwa serikali ya Palestina ilikubali kuichora upya mipaka ya Palestina na pia kutoruhusu zaidi ya wakimbizi milioni nne na nusu wa Kipalestina kurudi nyumbani.

https://p.dw.com/p/102kv
Mkutano wa Palestina na IsraelPicha: picture alliance/dpa

Ni shida kujua, Mamlaka ya Ndani ya Palestina inakanusha kipi na inakubali kipi kati ya yale yanayochapishwa na kituo cha Al-Jazeera chini ya kichwa cha maneno "Nyaraka za Palestina." Mwanzoni mkuu wa ujumbe wa upatanishi wa Palestina, Saeb Erakat, alikuwa akisema kwamba nyaraka hizi ni upotoshaji na uongo mtupu, huku Rais Mahmoud Abbas, akiziita upuuzi na njama za kuchanganya akili za watu, na sasa Erakat anasema zinasema nusu ya kweli, na kwamba hata kama yaliyomo yalizungumzwa hayakufikiwa makubaliano, ambayo baadaye yangelilazimika kupigiwa kura ya maoni na Wapalestina wenyewe.

Saeb Erekat
Saeb ErekatPicha: picture alliance/dpa

Miongoni mwa masuala makubwa, ambayo yamezusha hasira za Wapalestina wengi, ni lile la Erakat kukubaliana na sharti la kuruhusu wakimbizi laki moja tu wa Kipalestina kurudi nyumbani, kati ya milioni tano walosambaa katika nchi kadhaa za Kiarabu. Lakini Erakat anasema kwamba, katika mazungumzo yao, Israel ilitangaza kuchukua dhamana ya kushughulika na wakimbizi wapatao laki saba, ambao walilazimika kuikimbia nchi yao, baada ya mwaka 1948, taifa la Israel lilipoundwa, na kwamba msimamo wa serikali ya Palestina ni kwamba kila mkimbizi ataamua hatima yake mwenyewe.

Erakat asema Al Jazeera inazua

Erakat anadai kwamba Al-Jazeera inashirikiana na Israel na Marekani kuidhibu Palestina kwa uamuzi wa serikali ya nchi hiyo kupeleka kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, azimio la kuilaani Israel kwa kuendeleza ujenzi wa makaazi ya walowezi ya Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem ya Mashariki, na katika wakati huu ambao baadhi ya nchi za Marekani ya Kusini zikianza kuitambua dola ya Palestina na mipaka yake ya kabla ya vita vya mwaka 1967.

Palästinensische Arbeiter in der Pufferzone an der Grenze zwischen Gaza und Israel
Wafanyakazi wa Kipalestina mpakani mwa Gaza na IsraelPicha: DW/B.Marx

Akizungumza na AFP, Erakat aliituhumu Al-Jazeera kwa kujaribu kuwachochea Wapalestina wawapindue viongozi wao na kuuporomosha mfumo wa utawala wa Palestina. Alisema na hapa namnukuu: "Tupo kwenye hatua ya lalasalama kwenye mapambano yetu na tunaadhibiwa kwa sababu ya msimamo wetu." Mwisho wa kumnukuu.

Naye msaidizi mkuu wa Rais Mahmoud Abbas, Yasser Abd Rabb amesema kwamba, taarifa za Al-Jazeera ni sehemu ya mpango wa Amir wa Qatar Sheikh Hamad bin Khalifa al-Thani kuufelisha utawala wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Amesema kuwa amiri huyo ametoa idhini ya Al-Jazeera kufanya kampeni dhidi ya utawala wa Palestina.

Kituo cha habari cha Al-Jazeera kina makao yake makuu mjini Doha, nchini Qatar na Amir al-Thani ni miongoni mwa waanzilishi wake.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman