1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kasi ya UKIMWI yapunguwa Afrika

Mohamed Dahman14 Juni 2007

Kasi ya mripuko wa janga thakili la UKIMWI imekuwa ikipunguwa barani Afrika kutokana na jamii kuwezeshwa kujisaidia wenyewe kwa utaratibu mzuri wa kupatiwa kondomu na madawa ya kurefusha maisha kwa waathirika.

https://p.dw.com/p/CB3c
Watoto wenye virusi vya HIV nchini Ethiopia.
Watoto wenye virusi vya HIV nchini Ethiopia.Picha: AP Photo

Utafiti uliozinduliwa katika mji mkuu wa Rwanda Kigali umeonyesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la kupatikana nafasi ya kinga dhidi ya virusi vya HIV kwa mipango ya huduma na matibabu barani Afrika ambapo gonjwa hilo limeuwa zaidi ya watu milioni mbili mwaka jana wakati wengine milioni 25 wakiwa wameambukizwa na ugonjwa huo.

Waziri wa afya wa zamani wa Bhotswana na afisa mwandamizi ya Benki ya Dunia Joy Mphumaphi amesema katika taarifa kwamba UKIMWI umejipenyeza barani Afrika kama vile mwizi wakati wa usiku.

Amesema miaka mingi baadae bado inabidi waendele kuwa macho hata kama wakati inaonekana kwamba maambukizi yameanza kupunguwa na maisha ya watu wengi zaidi yamekuwa yakinusuriwa kwa kupatiwa matibabu.

Repoti hiyo ya Benki ya Dunia inasema mripuko wa gonjwa hilo la UKIMWI umeonyesha dalili za kupunguwa nchinim Uganda, Kenya na Zimbabwe kadhalika katika maeneo ya mjini nchini Ethiopia,Rwanda,Burundi,Malawi na Zambia.

Utafiti wa repoti hiyo umesema bila ya kutowa takwimu mahususi kwamba kuwaandaa na kuwawezesha kwa wananchi wa ngazi ya chini sambamba na kuwapatia mipira ya kondomu na matibabu ya madawa ya kurefusha maisha kwa waathirika kumeanza kupunguza kasi ya gonjwa hilo.

Hata hivyo repoti hiyo imeongeza kusema kwamba kusini mwa Afrika ni eneo linaloendelea kubakia kuwa kitovu cha ugonjwa huo kwa kuwa na kiwango kikubwa cha mambukizo kuwahi kushuhudiwa kabla.

Ikitaja uchunguzi wa hivi karibuni kwa familia katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Bhotswana wa Francistown umeonyesha asilimia ya kufadhaisha ya watu wenye virusi vya HIV ambayo ilikuwa ni asilimia 70 kwa wanawake wenye umri wa kati ya miaka 30-34 na wanaume kati ya umri wa miaka 40 na 44.

Utafiti huo ulikuwa ukitathmini matokeo ya mpango wa Benki ya Dunia wa miaka sita wa virusi vya HIV na UKIMWI kwa nchi mbali mbali uliogharimu dola bilioni moja nukta 28 ambao ulianzishwa hapo kwa 2000 kuongeza nafasi za mipango ya kuweza kupata kinga,huduma na matibabu.

Miongoni mwa shughuli nyengine mpango huo uliwapima takriban watu milioni saba katika nchi 25,ulisambaza karibu mipira ya kondomu bilioni moja na laki tatu na kuanzisha vituo vipya vya ushauri nasaha 1,500.

Mpango huo pia iligharimia makundi ya kijamii na vijana pamoja na mashirika ya watu wanaoishi na virusi vya HIV kadhalika kulipia madawa ya kurefusha maisha kwa watu 26,699 katika nchi 27.

Benki hiyo inasema kugharamia UKIMWI duniani kumeongezeka zaidi ya mara tatu kati ya mwaka 2001 na 2005 na kupindukia dola bilioni nane kwa mwaka.

Wiki iliopita katika Mkutano wa Viongozi wa Kundi la Mataifa Manane G8 uliofanyika nchini Ujerumani viongozi wa mataifa hayo tajiri kabisa duniani wameahidi kutowa dola bilioni 60 kupambana na UKIMWI barani Afrika juu ya kwamba ahadi hiyo haikutaja wakati wa kutolewa kwa fedha hizo.

Benki ya Dunia inasema virusi vya HIV na UKIMWI itaendelea kuwa changamoto kubwa kwa uchumi,jamii na binaadamu kusini mwa jangwa la Sahara kwa kipindi cha karibuni.

Kwa ujumla virusi vya HIV na UKIMWI vinatishia malengo ya maendeleo katika eneo hilo(kusini mwa jangwa la Sahara) kuliko mahali popote pale pengine duniani.