1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kasi ya ukuaji Uchumi Tanzania yapungua

Sylvia Mwehozi
12 Aprili 2017

Benki ya Dunia imesema kutokuwa na uhakika juu ya sera za serikali na kushuka kwa uwekezaji wa sekta binafsi kumepunguza kasi ya ukuaji wa pato la ndani nchini Tanzania hadi kufikia asilimia 6.9 mwaka 2016.

https://p.dw.com/p/2b6sr
Tansania John Pombe Magufuli Präsident
Picha: DW/S. Michael

Ukuaji wa uchumi bado unategemea uwekezaji muhimu wa serikali katika miundombinu ikiwemo reli ya kisasa, barabara mpya na upanuzi wa bandari.

Lakini wawekezaji wamekuwa na wasiwasi juu ya sera zisizotabirika katika serikali ya rais John Magufuli maarufu kwa jina la utani la Tingatinga kutokana na aina yake ya uongozi. Kuanguka kwa mzunguko wa fedha na mikopo isiyolipika pia vimezuia ukuaji wa mikopo wa sekta binafsi.

"Marekebisho ya sera yakitokea mara kwa mara yanaweza kusababisha kutokuwa na uhakika kwa sekta binafsi na wasiwasi huu unaweza kuogofya maamuzi ya uwekezaji ya sekta binafsi", inasema ripoti ya Benki Kuu ya Dunia kuhusu uchumi  wa Tanzania ya hivi karibuni.

Ripoti hiyo inapendekeza kwamba serikali inapaswa kuangalia kwa ukaribu, madhara yasiyotarajiwa ya sera za serikali kwa sekta binafsi.

Tansania Markt Bananen Verkauf
Ndizi zikiwa tayari kusafirishwa kwenda sokoni nchini Tanzania Picha: DW/V. Natalis

Inasema ukuaji uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2016 inawezekana ulipungua na kufikia asilimia 6.9, ikiwa ni tofauti kidogo chini ya matarajio ya serikali ya asilimia 7.2.

Mabenki nchini Tanzania yamejaribu kujikinga yenyewe kutokana na ongezeko la mikopo isiyolipika kwa kutengeneza mfumo wa viwango vya juu vya riba na kuongeza gharama za ukopaji.

Benki ya dunia inasema hatua za serikali za kupunguza matumizi na gharama, ikiwemo kuwazuia maafisa wa serikali kusafiri nje ya nchi zinaweza kuathiri sekta binafsi.

"Vikao vya serikali vilivyokuwa vikifanyika katika hoteli za kitalii vimepigwa marufuku, hii ni mojawapo ya mfano wa mageuzi ya serikali ambayo yameleta athari kwa sekta binafsi, ambayo inategemea mahitaji ya serikali", imesema ripoti hiyo.

Baada ya kuingia madarakani Novemba 2015, Rais Magufuli alianzisha vita dhidi ya wakwepa kodi hasa akiyalenga makampuni makubwa. Baadhi ya wawekezaji wa kigeni wanasema wameshindwa kuendelea na oparesheni au kupanua mipango yao kwa sababu ya mahitaji magumu yaliyowekwa dhidi ya makampuni ikiwemo tuzo za juu za kodi.

Benki ya dunia inapendekeza kwamba kwa viashiria hivi hasi katika biashara kunahitajika serikali kufanya mjadala na sekta binafsi juu ya mazingira ya uwekezaji.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Josephat Charo