1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katika magazeti ya leo

Maja Dreyer25 Oktoba 2007

Mada zinazozingatiwa leo na wahariri wa magazeti ni mbali mbali. Moja kati ya hizo ni msimamo wa Uturuki katika suala la Wakurdi na uhusiano wake na Iraq.

https://p.dw.com/p/C7lB

Kwanza katika udondozi wa magazeti hii leo tunalisikia gazeti la “Berliner Zeitung”:

“Kinachoendelea hivi sasa ni mjadala kuhusu sera za msingi za Uturuki. Ikiwa Uturuki inaelekea kuwa na mamlaka fulani katika eneo hili, washirika gani na sera gani zitaisaidia kutumia ushawishi wake? Marekani na mbinu yake ya kujiingiza katika mambo ya ndani ya nchi nyingine inaweza ikailetea Uturuki shida kuliko faida. Serikali ya Uturuki itanufaika zaidi kwa kuwa na usalama katika eneo zima. Nani basi tena: Urusi? China? India? Inaonekana kama Uturuki inaelekea njia mpya kabisa katika sera zake.”

Tukibakia kidogo kwenye mada hiyo, tupate pia uchambuzi wa “Südwest-Presse” juu ya mbinu ya Uturuki kuelekea Wakurdi. Gazeti limeandika:

“Uturuki ina tuhuma na wasiwasi juu ya kujengwa kwa jamii ya Wakurdi nchini Iraq waliokuwa na serikali yao ya ndani ikihofia kwamba Wakurdi wanaoishi Uturuki watataka mfumo huo huo. Mashambulizi mengine ya wanamgambo wa Kikurdi wa PKK yataipa Uturuki sababu nzuri za kuivamia Iraq na kutaathiri usalama miongoni mwa Wakurdi.”

Aidha kwenye kurasa za wahariri ni mkutano wa shirika la kujihami la Magharibi NATO uliofanyika jana nchini Uholanzi. Gazeti la “Kölnische Rundschau” linachambua hali ya ndani ya shirika hilo:

“Hali ya mvutano katika ushirikiano huu wa nchi za Magharibi inaonyesha ni tatizo la msingi la NATO ambalo pia ni tatizo la Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa. Jumuiya hizo zote yanajaribu kutuliza mizozo mingi iliyotokea ulimwenguni. Lakini kwa vile mizozo ni mingi – Afghanistan, Kosovo, Sudan, Libanon, Kongo, Somalia na Chad – uwezo hautoshi tena. Nchi za magharibi zimejibebesha mizigo kuzidi kiasi.”

Katika matangazo yetu ya hivi karibuni tulizungumzia mfumo mpya wa kudhibiti uhamiaji barani Ulaya uliopendezwa na Umoja wa Ulaya kwa jina la “Blue Card”. Lengo ni kuwa na mfumo wa pamoja utakaowavutia hasa wataalam kuja Ulaya na kufanya kazi. Serikali ya Ujerumani pamoja na nchi nyingine za Umoja huu zinapinga kuanzishwa kwa “Blue Card”. Mhariri wa “Stuttgarter Zeitung” lakini ana maoni tofauti:

“Mfumo huu wa “Blue Card” utasaidia kuzifanya nchi za Umoja wa Ulaya kuwa pahali pazuri pa kufanya kazi. Hoja zilizotolewa na serikali ya Ujerumani dhidi ya “Blue Card”, kwa kweli, hazieleweki. Pendekezo la Umoja wa Ulaya linasisitiza kwamba idadi ya “Blue Card” itawekwa na kila nchi wanachama. Historia inatufundisha kwamba serikali za kitaifa kusimamia uhamiaji peke zao hakufai, kwani kila mara nchi moja ilipobadilisha sheria zake za uhamiaji, hatua hiyo inaziathiri nchi nyingine za Umoja huu ambao haudhibiti mipaka yake ya ndani. Kwa hivyo inabidi kuwa na suluhisho la pamoja.”

Hatimaye ni mhariri wa “Landeszeitung Lüneburg” ambaye anatafuta sababu ya kutokea moto kmubwa huko California, Marekani, na anasema maafa hayo yalisababishwa na binadamu. Ameandika:

“Jiji la Los Angeles ambalo zamani lilikuwa kijiji kidogo halingeweza kukua hivi bila ya kutumia mto wa Owens kwa kujenga bomba kubwa zaidi duniani. Lakini bomba hilo ilisababisha pia maeneo yanayozunguka Los Angeles kukauka. Kuzima moto inabakia kuwa hatua ndogo na mara nyingi sababu ni kosa la mwanadamu.”