1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kemikali Ali ahukumiwa kifo

Mohamed Dahman24 Juni 2007

Mahkama ya Baghdad imemhukumu kifo kwa kunyongwa Ali Hassan al –Majid ambaye maarufu kwa jina la Kemikali Ali kwa mauaji ya kimbari,uhalifu dhidi ya ubinaadamu na uhalifu wa vita.

https://p.dw.com/p/CB3L
Ali Hassan al- Majid akisikiliza kesi yake kizimbani.
Ali Hassan al- Majid akisikiliza kesi yake kizimbani.Picha: picture-alliance/dpa

Wanachama wengine wawili wa zamani wa ngazi ya juu katika utawala wa Saddam Hussein pia wamehukumiwa adhabu ya kifo kwa dhima waliyotimiza katika shambulio la mauaji ya kimbari dhidi ya Wakurdi walio wachache nchini Iraq.Watu wengine wawili wamehukumiwa kifungo cha maisha gerezani na mtu wa watano ameachiliwa huru kutokana na kukosekana kwa ushahidi.

Ali Hassan al Majid binamu wa Saddam Hussein amekuwa akihesabiwa kuwa ni mpangaji wa kampeni hiyo ya mauaji ya kimbari.Ametuhumiwa kwa kuamuru mashambulizi hayo kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya wananchi wa Kikurdi walioko kaskazini mwa Iraq na kupelekea vifo vya takriban Wakurdi 180,000.