1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kuwajengea nyumba wanajeshi wake

Mohammed Khelef
16 Desemba 2021

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amezindua mradi wa ujenzi wa nyumba za wanajeshi wa vikosi vya ulinzi katika miji mitano ya nchi hiyo kwa wakati mmoja ili kuboresha hali yao ya maisha.

https://p.dw.com/p/44NMB
Uhuru Kenyatta Präsident Kenia Rede Parlament Nairobi
Picha: Simon Maina/AFP via Getty Images

Mradi huo unaotekelezwa kwa ushirikiano wa sekta za kibinafsi na umma unaanza kwa ujenzi wa nyumba  3,500 katika awamu ya kwanza.

Akizungumza wakati wa sherehe ya kuweka jiwe la msingi katika kambi ya kijeshi ya Roysambu jijini Nairobi, Rais Uhuru Kenyatta amesema mradi wenyewe utakamilika kwa muda wa miaka miwili.

Mradi huo unaambatana na aJEnda nne kuu za serikali, hasa lengo la kutoa makaazi ya gharama nafuu.

Nyumba hizo zitakabidhiwa kwa wanajeshi kwa misingi ya kujengwa, kukodishwa na kuhamishwa.

Zitajengwa kwenye ardhi ya kambi ya Roysambu jijini Nairobi, Nanyuki, Gilgil kaunti ya Nakuru na Nyali jijini Mombasa.

Kenia Wahlen Unruhen Polizei gegen Demonstration der Opposition in Kisumu
Askari wa KenyaPicha: AP

Mkuu wa majeshi ya Kenya, Jenerali Robert Kibochi ameeleza kwamba limekuwa azimio la muda mrefu kuwa na makaazi ya pamoja ya wanajeshi hasa kwa ajili ya kurahisisha huduma yao.

Pamoja na hayo, Rais Kenyatta alisema serikali inanuia kujenga na kuimarisha hospitali za kijeshi ili kuweza kuwahudumia vyema zaidi wanajeshi na familia zao kote nchini.

Wakati huo huo, serikali kupitia Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang'i, imetangaza kusitishwa kwa likizo zote kwa maafisa wa usalama msimu huu wa Sherehe za Krismasi, wale walio likizoni wakitakiwa kurejea kazini mara moja.

"Kenya inaazimia kuimarisha hali ya usalama hasa ikizingatiwa kuwa mataifa jirani ya Ethiopia na Somalia yamekuwa yakishuhudia msukosuko wa kiusalama." Alisema waziri huyo.
 

Imeandikwa na Wakio Mbogho, DW Nakuru