1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yatamba Osaka

Ramadhan Ali28 Agosti 2007

Kenya ilitoroka leo na mbili za dhahabu katika mita 800 wanawake na mita 3000 kuruka viunzi wanaume.Dibaba wa ethiopia ajitoa katika mbio za mita 5000 wanawake.

https://p.dw.com/p/CHb8
Janeth Jepkosgai anashangilia ushindi wake
Janeth Jepkosgai anashangilia ushindi wakePicha: AP Photo/David J. Phillip

Baada ya kunyakua medali ya dhahabu katika mbio za marathon na jana kuondoka na medali 2 za shaba-moja katika mita 10.000 na nyengine mita 3000 kuruka viunzi wanawake, leo imetoroka na medali nyengine mbili za dhahabu katika mita 800 wanawake na mita 3000 wanaume kuruka vinzi-steeplechase.

Bingwa wa Jumuiya ya madola na wa Afrika katika masafa ya mita 800,mkenya Janeth Jepkosgei aliipatia Kenya medali yake ya kwanza kabisa ya mita 800 katika mashindano ya riadha ya dunia.

Akishika usukani wa mbio hizo kuanzia mwanzo hadi mwisho,Janeth alishinda kwa muda wake wa dakika 1.sek.56.4.huo ndio muda bora kabisa mwaka huu.Nafasi ya pili alifuata mmorocco Hasna Benhassi aliechukua dakika 1:56.99.Alifuatwa nafasi ya 3 na mspain Mayte Martinez.

Maria Mutola wa Msumbiji aliekuwa akisaka medali yake ya 8 ya dhahabu ya ubingwa wa dunia alijitoa mbioni masafa mafupi kabla kumaliza mbio hizo akishindwa kukamata mkenya Janeth Jepkosgei.

Haya bila shaka yatakua ni mashindano ya mwisho ya ubingwa wa dunia kwa maria Mutola wa Msumbiji.Alishinda 1993,2001 na tena 2003.

Hiyo haikuwa medali pekee ya dhahabu leo kwa Kenya.

Katika finali ya mita 3000 kuruka viunzi ambamo Kenya inadai ni mali yake, imezowa medali zote 3-dhahabu,fedha na shaba.Ilikua Brimin Kipruto,bingwa wa medali ya fedha wa Olimpik na sio Ezekiel Kemboi aliewaongoza wakenya kuzowa medali zote 3.

Kipruto alimpita wazi Kemboi mnamo mita 150 za mwisho na kunyanyua mikono juu akishinda kwa muda wake wa dakika 8. sek.13.82.

Kermboi alibidi kuridhika na medali ya fedha huku ile ya shaba ikienda kwa Richard Mateelong.

Mwishoe,akifurahia ushindi wake wa leo, Kipruto alisema ,”hii ni mara yangu ya kwanza nashinda medali ya dhahabu.Tutasherehekea leo kama timu moja na kama nchi moja.”

Bingwa wa mita 10.000 wanawake kutoka Ethiopia, Tirunesh Dibaba amejitoa katika changamoto ya mita 5000 akihisi maumivu ya tumbo bado yanamsumbua.Kwa hatua hiyo hataania kutwaa mataji yote 2-mita 10.000 na 5000 kama alivyokusudia.

Ethiopia sasa inawakilishwa na wasichana wengine hatari Meseret Defar,Meselech Melkamu na Gelete Burka.Wote watahakikisha kwamba medali ya dhahabu ya mita 5000 inarudi Adis Ababa.

Muestonia Gerd Kanter alikomesha leo enzi ya miaka 7 ya bingwa wa kurusha kisahani cha chuma-discus ya Alekna.Kanter alirusha kisahani hicho masafa ya mita 68.94 ili kunyakua medali ya dhahabu kwa Estonia.

Mjerumani Robert Harting, alimaliza wapili kwa masafa yake ya mita 66.68 na kuondoka na medali ya fedha.Medali ya dhahabu, ilikwenda pia kama ilivyotazamiwa kwa msichana wa kirusi Isinbayeva,bingwa wa rekodi kadhaa katika kuruka kwa upongoo (Pole Vault).Mashindano ya riadha ya dunia mjini Osaka,Japan, yanaendelea hadi Septemba 2 na wanariadha wa Afrika na hasa Kenya na Ethiopia wanaendelea nao kutamba.