1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta aapishwa, Odinga asusa

Mohammed Khelef
28 Novemba 2017

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameapishwa kwa muhula mwengine, huku hasimu wake mkuu, Raila Odinga, akiapa kutomtambua na akikusudia kujiapisha mwenyewe kuwa rais wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

https://p.dw.com/p/2oP9G
Kenia Amtseinführung Präsident Kenyatta
Picha: Reuters/T. Mukoya

Maelfu ya wafuasi wa chama tawala cha Jubilee kinachoongozwa na Kenyatta na makamu wake, William Ruto, walimiminika kwenye uwanja wa mpira wa Kasarani tangu nyakati za asubuhi kumshuhudia milionea huyo mwenye umri wa miaka 56 akila kiapo cha kuhudumu muhula wake wa pili.

Katika hotuba yake, mara baada ya kula kiapo, Kenyatta aliahidi kuuziba ufa wa kisiasa uliotokana na chaguzi zilizopita - ule wa Agosti 8 ambao matokeo yake yalifutwa na Mahakama ya Juu na huu wa Oktoba 26 ambao kwa mara nyengine ulimpa ushindi mkubwa, kufuatia kugomewa na upinzani.

"Nitajitolea muda na nguvu zangu zote kujenga madaraja ya kuwaunganisha Wakenya na kuleta maendeleo," alisema Kenyatta kwenye hotuba hiyo. 

Pia alitambua madhara makubwa yaliyotokana na siasa za Kenya, akipigia mifano kwenye matokeo kadhaa ya machafuko kabla ya kuapishwa kwake. 

"Tumeshikilia siasa kama ndilo lengo lenyewe, badala ya kuwa njia ya kutufikisha kwenye lengo la ustawi wa kiuchumi. Hili lazima likomeshwe mara moja," aliwaambia waliohudhuria.

Odinga asema 'ataapishwa'

Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.
Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Usalama uliimarishwa kwenye uwanja huo na maeneo mengine ya mji mkuu, Nairobi, huku wafuasi wa muungano wa upinzani (NASA) wakikabiliana na polisi katika eneo la Jakaranda, kando kidogo ya kitovu cha jiji hilo.

Kiongozi wa NASA, Raila Odinga, aliwaambia wafuasi wake kwamba "ataapishwa" kuwa rais tarehe 12 Disemba. Alitoa kauli hiyo akiwa kwenye ibada ya kuwakumbuka wale waliouawa na polisi kwenye kipindi cha uchaguzi.

"Tarehe 12 Disemba tunazindua bunge letu la watu na bunge hilo ndilo ambalo litaniapisha mimi," alisema.

"Tutaapishwa kama Mnangagwa (rais mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa) na tutakwenda sambamba na katiba," alisisitiza Odinga. 

Bado haijawa wazi nini kitafanyika ndani ya siku chache zijazo kufuatia madai hayo ya upinzani ya kutomtambua Kenyatta na kutaka kujipisha wenyewe, lakini kwa vyovyote vile ishara si njema.

Kuingia madarakani kwa Kenyatta katika awamu hii ya pili kumekumbana na mpasuko mkubwa zaidi wa kijamii na kisiasa kuwahi kushuhudiwa na taifa hilo lenye nguvu zaidi kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman