1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry ataka mazungumzo ya Kampala yaharakishwe

Admin.WagnerD25 Septemba 2013

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amekutana na rais Joseph Kabila, na kuelezea umuhimu wa kurejesha amani katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo haraka.

https://p.dw.com/p/19oYo
Waziri John Kerry akiwa na rais Joseph Kabila mjini New York siku ya Jumatano.
Waziri John Kerry akiwa na rais Joseph Kabila mjini New York siku ya Jumatano.Picha: DW/ S. Mwanamilongo

Kerry amesema mazungumzo ya Kampala baina ya serikali ya Kongo na waasi ni lazima yafaulu. Waziri Kerry alisema nchi yake inataka kuona amani imerejea kwa manufaa ya wananchi wa Kongo. “Cha muhimu kwa raia wa Kongo na wale wa kanda la maziwa makuu ni kuweko na amani na ustawi.Tunatumaini katika kufanikisha hilo,na tunategemea kufanya kazi pamoja na rais Kabila na viongozi wengine wa kanda hilo ilikufanikisha juhudi za amani," alisema Kerry.

John Kerry alisema Marekani itaendelea kuunga mkono juhudi zote za amani ilikumaliza makundi ya wapiganaji yalioko mashariki mwa Kongo.Kerry alisema wanategemea pia kufaulu kwa mazungumzo ya amani ya Kampala baina ya serikali ya Kongo na kundi la waasi la M23.

“Mimi na rais Kabila tulikuwa na mazungumzo muhimu kuhusu matatizo ya kanda la maziwa makuu,na vilevile kutafakari kuhusu kufaulu kwa mazungumzo ya Kampala.Tunatumaini kuna njia baina yetu na mjumbe maalumu wa Marekani Russ Feingold yakuunga mkono juhudi hizo iliamani iweko”.

Wanajeshi wa kundi la uasi la M23, ambalo linapambana na serikali ya Kongo.
Wanajeshi wa kundi la uasi la M23, ambalo linapambana na serikali ya Kongo.Picha: Melanie Gouby/AFP/GettyImages

Mwezi julai mwaka huu, waziri John Kerry aliitisha mkutano wa ngazi ya juu kwenye baraza la usalama la umoja wa mataifa ilikujadili mzozo wa Kongo. "Tunapiga hatua kidogo lakini haitoshi, tunajaribu kufikia mwisho wa mazungumzo ya kampala .Natunatumaini kufikia amani, lakini inahitaji kufanya kazi zaidi kwa sababu kuna mengi ya kufanya katika kujenga amani hiyo,” alisema Kerry.

John Kerry ambae alikutana na rais Joseph Kabila kwa zaidi ya dakika 45 alisema Marekani itaendelea kubakia kuwa mshirika mkuu wa nchi za maziwa makuu katika maendeleo yake. Msimamo huo aliutoa baada ya mkutano wa ngazi ya juu ulioitishwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika mjini NewYork kujadili amani ya Kongo.

Mkutano huo uliowajumlisha marais na viongozi wa serikali wacnchi 11 za kanda ya maziwa makuu ulitoa mwito wa kukamilisha mazungumzo ya Kampala bila kupoteza muda wowote. Rais Joseph Kabila alihutubia Umoja wa Mataifa katika mkutano mkuu wa mwaka, hotuba ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa nchini Kongo kutokana na mazungumzo ya kitaifa, juhudi za amani na vilevile uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.

Mwandishi: saleh Mwanamilongo
Mhariri: Josephat Charo