1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry kuishinikiza Uturuki kuhusu uhusiano na Israel, Syria na Iraq

7 Aprili 2013

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amewasili nchini Uturuki, katika ziara iliyozingwa na mauaji ya mwanadiplomasia wa kike katika shambulio la bomu nchini Afghanistan.

https://p.dw.com/p/18B7x
John Kerry mjini Ankara
John Kerry mjini AnkaraPicha: ADEM ALTAN/AFP/Getty Images

Kerry aliwasili mjini Istanbul wiki mbili baada ya rais wa Marekani Barack Obama kunadi maridhiano kati ya Uturuki na Israel, ambazo uhusiano wake uliharibiwa na mauaji ya raia tisa wa Uturuki katika tukio la uvamizi dhidi ya meli ya misaada ya Uturuki na jeshi la majini la Israel mwaka 2010. Maridhiano hayo huenda yakasaidia uratibu wa kikanda kuzuia kusambaa kwa mgogoro wa Syria na kulegeza kutengwa kidiplomasia kwa Israel katika mashariki ya kati, wakati taifa hilo la kiyahudi likikabiliwa na changamoto za programu ya nyuklia ya Iran.

Rais Barack Obama akimtambulisha waziri John Keryy kwa rais wa Israel Shimon Perez.
Rais Barack Obama akimtambulisha waziri John Keryy kwa rais wa Israel Shimon Perez.Picha: Reuters

Licha ya Obama kufanikiwa kurejesha mawasiliano kati ya mawaziri wakuu wa Israel na Uturuki, ambao walikuwa hawajazungumza tangu mwaka 2010, kupitia mawasiliano ya simu ya pande tatu ya Machi 22, utawala mjini Washington una wasiwasi kuwa huenda Uturuki inataka kujiondoa katika makubaliano hayo. Israel ilisalimu kwa madai ya muda mrefu ya Uturuki, ambayo iliwahi kuwa mshirika wake muhimu, kuomba radhi rasmi kutokana na vifo vilivyotokea ndani ya Meli ya Uturuki ya Mavi Marmara.

Meli hiyo ilipandwa na wanamaji wa Israel ambao walizuia kundi dogo la vyombo vya majini vilivyokuwa vinakiuka vizuizi vya Israel dhidi ya ukanda unaoogozwa na chama cha Hamas wa Gaza. Ofisi ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema kuwa alikubali kukamilisha makubaliano juu ya fidia, na kwamba waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikubali kurejesha uhusiano, ikiwemo kuwarejesha mabalozi katika vituo vyao.

Afisa wa ngazi ya juu wa Marekani aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa wanasifiri na Kerry kuwa alisema ataihimiza Uturuki kutekeleza makubaliano yake na Israel na kurejesha kamili uhusiano baina ya mataifa hayo mawili. Wakati afisa huyo alikanusha kuwa Marekani ina wasiwasi kuwa serikali ya Uturuki inaweza kuwa inajitenga na makubaliano hayo, afisa mwingien wa Marekani alisema mapema wiki hii kuwa utawala mjini Washington ulikuwa na wasiwasi.

Wakimbizi wa Syria walioko mpakani mwa Uturuki na Syria.
Wakimbizi wa Syria walioko mpakani mwa Uturuki na Syria.Picha: BULENT KILIC/AFP/Getty Images

Changamoto ya wakimbizi

Kerry pia ataibua masuala ya Syria na Iraq wakati wa mazungumzo yake na na Waziri Mkuu Erdogan na waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Ahmet Davutoglu mjini Istanbul, kituo chake cha kwanza katika ziara hii ya siku kumi mashariki ya kati, Ulaya na Asia. Motisha muhimu ya maridhiano kati ya Israel na Uturuki, angalau kwa upande wa Israel, ni hamu ya kupata washirika katika kanda, wakati ambapo vita vya Syria vinaingia katika mwaka wake wa tatu.

Ujumbe wa Kerry kwa Instanbul utahusisha kurudia umuhimu wa kuacha mipaka wazi kwa wakimbizi kutoka Syria, afisa mwandamizi aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa na Kerry. Hii ni kutokana na ripoti zilizokanushwa na Uturuki Machi 28, kwamba iliwakusanya na kuwarudisha mamia ya wakimbizi wa Syria kufuatia machafuko katika kambi ya mpakani.

Mashuhuda walisema mamia ya wakimbizi waliwekwa ndani ya mabasi na kupelekwa mpakani baada ya kutokea makabiliano, ambapo wakimbizi katika kambi ya Suleymanansah, karibu na mji wa Uturuki wa Akcakale, waliwarushia mawe polisi jeshi, ambao nao walijibu kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na mabomba ya kutoa maji kwa kasi.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki ilisema watu 130 waliotambuliwa kama washiriki wa fujo hizo, walivuka mpaka na kurudi nchini Syria kwa hiari yao, ama kwa sababu hawakutaka kukabiliana na sheria, au kwa sababu ya kuhofia kisasi kutoka kwa wakimbizi wengine. Tukio hilo lilibainisha kero inayosababishwa na wakimbizi wa Syria kwa mataifa jirani.

Waziri John Kerry akiwa mjini Ankara, Uturuki.
Waziri John Kerry akiwa mjini Ankara, Uturuki.Picha: ADEM ALTAN/AFP/Getty Images

Tangu kuanza mgogoro huo miaka miwili iliyopita, zaidi ya wasyria milioni 1.2 wanaokimbia vurugu na mateso wamejiandikisha kama wakimbizi au wanasubiri kuandikishwa katika mataifa ya jirani, na Afrika Kaskazini, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. Wanahusisha 261,635 waliopo nchini Uturuki, wengi wao wakiishi katika kambi 17, ambazo nyingi zimejaa.

Uhusiano na Iraq, na amani ya mashariki ya kati

Kerry pia anatarajiwa kuishinikiza Uturuki kuboresha uhusiano wake na Iraq, ambayo inatatizika na juhudi za mkoa huru wa Kurdistan, ambako watu wa kabila la Wakurd wamekuwa wakijitawala tangu mwaka 1991, kuiuzia nishati Uturuki. Serikali kuu ya Iraq inasema jambo hili litakuwa linaikosesha mapato ya mafuta, ambayo ni ya nchi nzima.

Baada ya mazungumzo nchini Uturuki, Kerry ataelekea baadae leo nchini Israel na mjini Ramallah, katika ukingo wa Magharibi, ambako atakutana na rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas. Atakutana pia na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumatatu, katika kile ambacho kitakuwa ziara yake ya tatu katika kanda ya mashariki ya kati tangu aanze kazi yake Februari mosi.

Maafisa wa Marekani wanasema ziara hiyo nyingine itampa nafasi kuangalia uwezekano wa kuanzisha tena mazungumzo ya amani, ambayo yalikwama kwa miaka zaidi ya miwili, kufuatia ziara ya Obama mwezi uliyopita. Safari ya Kerry kuelekea mjini Istanbul ilicheleweshwa kwa karibu masaa matatu, baada ya mlango wa ndege yake aina ya Boeing 757 kuharibika, na alihuzunishwa na msiba nchini Afghanistan, wakati akisubiri na mkewe Tereza Heinz Kerry kuletewa ndege nyingine.

Rais Barack Obama akimtambulisha waziri John Keryy kwa rais wa Israel Shimon Perez.
Waziri Kerry akiwa na waziri mkuu wa Iraq, Nouri al-Maliki, alipoizuru nchi hiyo mwezi uliyopita.Picha: Reuters

Kabla ya kuondoka, aliwapigia simu wazazi wa mfanyakazi wa wizara yake kuwapa pole. Mfanyakazi huyo, ambaye Kerry alikutana naye mwezi uliyopita alipotembelea mjini Kabul, alifariki siku ya Jumamosi katika shambulio la bomu la barabarani dhidi ya msafara wa Jumuiya ya Kujihami NATO, katika mkoa wa Zabul, ambalo liliwauwa wanajeshi watatu wa NATO na raia wawili.

Shambulio la Zabul, limekuja karibu miezi saba kamili baada ya balozi Chris Steven na wamarekani wengine watatu kuuawa katika shambulio la kijeshi Septemba 11 dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe,rtre
Mhariri: Bruce Amani