1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry na Lavrov kukutana

14 Machi 2014

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry leo (14.03.2014) anatarajiwa kukutana na waziri mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, katika juhudi za kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/1BPey
John Kerry akiwa na Sergei Lavrov
John Kerry akiwa na Sergei LavrovPicha: Reuters

Mkutano huo unafanyika huku mataifa ya Magharibi yakiwa tayari kuiwekea Urusi vikwazo vikali, kutokana na nchi hiyo kuchochea ghasia na kuipinga serikali mpya ya Ukraine.

Mkutano wa Kerry na Lavrov unafanyika mjini London, Uingereza kwa lengo la kutuliza mzozo uliopo kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni kama Crimea ijiunge na Urusi au ibakie kuwa sehemu ya Ukraine, iliyopangwa kufanyika Jumapili ijayo. Wanadiplomasia hao wanakutana baada ya hivi karibuni kushindwa kuweka kando tofauti zao kuhusiana na mzozo wa Ukraine.

Akizungumza jana Alhamisi (13.03.2014) na jopo la maseneta wa Marekani, Kerry alisema kuwa Urusi itarajie Marekani na Umoja wa Ulaya kuchukua hatua dhidi yake Jumatatu ijayo, kama Urusi itakubaliana na uamuzi wa Crimea kujitenga kutoka Ukraine. Marekani na Umoja wa Ulaya zinasema kura hiyo inakiuka katiba ya Ukraine na sheria za kimataifa. Hata hivyo, Urusi imesema itaheshimu matokeo ya kura hiyo ya maoni.

Arseniy Yatsenyuk akiwa na Rais Barack Obama
Arseniy Yatsenyuk akiwa na Rais Barack ObamaPicha: picture alliance / AP Photo

Matamshi ya Kerry yanaunga mkono kauli iliyotolewa na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ambaye alisema Urusi iko katika hatari ya kukabiliwa na athari za kiuchumi na kisiasa, iwapo itakataa kulegeza msimamo wake dhidi ya serikali mpya ya Ukraine.

Marekani yaiunga mkono Ukraine

Katika kuonyesha kuiunga mkono Ukraine, Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, jana alikutana na Waziri Mkuu, Arseniy Yatsenyuk, siku moja baada ya kiongozi huyo wa Ukraine kukutana na Rais Barack Obama, mjini Washington. Hata hivyo, Urusi na Ukraine zimesisitiza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba hazitaki vita na bado upo uwezekano wa kuutatua mzozo wa Ukraine kwa njia za amani.

Yatsenyuk alisema ikiwa mazungumzo ya kweli na Urusi yatafanyika, nchi hizo mbili zinaweza kuwa washirika.

Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin
Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vitaly ChurkinPicha: REUTERS

Kwa upande wake Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, aliliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba nchi yake inataka kufanya mazungumzo na Ukraine na hawataki aina yoyote ya uchokozi wa kijeshi. Urusi imetuma wanajeshi wake katika eneo la Crimea, kabla ya kufanyika kwa kura hiyo ya maoni.

Wakati huo huo, kijana mwenye umri wa miaka 22, anayeiunga mkono serikali ya Ukraine, ameuawa katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo. Mauaji hayo yametokea katika maandamano ya wafuasi wanaoiunga mkono Urusi na wale wanaoipinga.

Ama kwa upande mwingine masoko ya hisa ya Urusi leo yameshuka kwa asilimia tano, kutokana na wawekezaji kuwa na hofu kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni siku ya Jumapili.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman